Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa akionyesha begi lililobeba hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013, wakati akielekea kuingia katika ukumbi wa Bunge, mjini Dodoma jana.
SERIKALI jana ilitangaza Bajeti ya Sh15trilioni kwa mwaka wa fedha
2012/2013 ambayo pamoja na mambo mengine, imelenga kudhibiti mfumuko wa
bei kwa kutangaza kutoa vibali vya kuingiza chakula kutoka nje, huku
ikiwabana matajiri kwa kuongeza kodi ya bidhaa zisizokuwa za lazima.
Akisoma bajeti hiyo bungeni Dodoma jana, Waziri wa Fedha, Dk William
Mgimwa alitangaza pia kwamba Serikali imepanua wigo wa Kodi ya Mishahara
(Paye) na sasa itawagusa wafanyakazi wenye kipato cha kuanzia Sh170,000
badala ya Sh135,000 ya awali, huku ikirejesha mafunzo ya Jeshi la
Kujenga Taifa (JKT) kwa kutenga Sh7 bilioni kwa ajili ya kuchukua vijana
5,000.
Dk Mgimwa katika Bajeti hiyo pia alitangaza ongezeko la kodi za bidhaa
mbalimbali, ikiwamo, bia, soda, sigara, juisi zinazoingizwa kutoka nje
huku ikifuta msamaha wa ushuru wa bidhaa kwa magari kwa wote waliokuwa
wananufaika na msamaha huo.
Alifafanua kwamba kodi ya vinywaji baridi imepanda kutoka Sh69 kwa lita
hadi Sh83 na mvinyo unaotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nchini kwa
kiwango kinachozidi asilimia 75, imeshuka kutoka Sh425 kwa lita hadi 145
kwa lita.
Kodi ya mvinyo unaotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa
kiwango kinachozidi asilimia 25, imepanda kutoka Sh1,345 kwa lita hadi
1,614 kwa lita.
Alisema kodi ya vinywaji vikali imepanda kutoka Sh1,993 kwa lita hadi
Sh2,392 kwa lita, bia inayotengenezwa nchini kwa nafaka na ambayo
haijaoteshwa, kodi yake imepanda kutoka Sh248 kwa lita hadi Sh310 kwa
lita. Bia nyingine zote kodi imepanda kutoka Sh420 hadi Sh525 kwa lita.
Akizungumzia
marekebisho ya ushuru kwenye bidhaa za sigara, Dk Mgimwa alisema zote
zisizo na kichungi na zinazotengenezwa kwa tumbaku inayozalishwa nchini,
kiwango cha angalau asilimia 75, kodi imepanda kutoka Sh6,820 hadi Sh
8,210 kwa sigara 1,000.
Alisema Sigara zenye kichungi na
zinazotengenezwa kwa tumbaku inayopatikana nchini kwa kiwango cha
angalau asilimia 75, kodi imepanda kutoka Sh16,114 hadi Sh19,410 na
sigara nyingine zenye sifa tofauti na makundi hayo, kodi imepanda kutoka
Sh29,264 hadi Sh35,117 kwa sigara 1,000.
Alisema tumbaku ambayo
ipo tayari kutengenezwa sigara (cut filler) kodi yake imepanda kutoka
Sh14,780 hadi Sh17,736 kwa bunda la sigara 1,000 wakati ushuru wa cigars
unabaki kuwa asilimia 30.
Gharama za simu juu
Katika bajeti
hiyo, Waziri Dk Mgimwa alisema muda wa maongezi (airtime) kwenye simu za
mkononi umeongezeka kutoka asilimia 10 hadi 12.
Alisema lengo la
hatua hiyo ni kuoanisha ushuru wa bidhaa unaotozwa na huduma hiyo katika
nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC), kwa kipindi hiki ambacho
nchi zipo katika Soko la Pamoja.
Alisema hatua hizo za ongezeko la
ushuru wa bidhaa kwa pamoja, zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali
kwa kiasi cha Sh144,054.9 milioni.
Misamaha ya kodi ya magari
Waziri
huyo alipendekeza kufanyika marekebisho kwenye sheria husika za kodi ya
matangazo ya Serikali yanayotoa msamaha wa kodi kwenye magari kwa
walengwa mbalimbali ili kuweka ukomo wa umri wa miaka minane kwa magari
hayo badala ya miaka 10.
Alisema magari yenye umri wa zaidi ya
miaka minane yatatozwa ushuru wa bidhaa wa asilimia 20. Lengo la hatua
hiyo ni kupunguza wimbi la uingizaji magari chakavu na kulinda
mazingira.
Alitangaza pia marekebisho katika ushuru wa forodha,
ikiwemo kufuta msamaha wa ushuru wa forodha katika vitu mbalimbali
vikiwemo magari yenye ujazo wa CC 3000 huku pia ushuru wa forodha
ukifutwa katika bidhaa nyingine nyingi muhimu.
Alisema katika kuhamasisha na kuchochea ukuaji wa sekta ya ufugaji wa
nyuki, vifaa vinavyotumika katika ufugaji na kurina asali vimepewa
msamaha wa ushuru wa forodha vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi na
wafugaji wa nyuki.
Alisema msamaha wa ushuru wa forodha kwenye migahawa ya majeshi ya ulinzi utaendelea kutolewa kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Alisema kumefanyika
marekebisho katika Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki
ya mwaka 2004 ili kutoa msamaha wa ushuru wa forodha kwa wazalishaji wa
vyakula vinavyotengenezwa mahsusi kwa lishe ya watoto wenye utapiamlo na
watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi.
Alisema kuwa katika Bajeti
hiyo, pia wametoa msamaha wa ushuru wa forodha kwenye malighafi
zinazotumika katika kutengeneza vifaa vya kufanyia uchunguzi wa magonjwa
(medical diognastic kits) kwa kuwa vifaa hivyo hutozwa asilimia sifuri
vinapoagizwa kutoka nje ya nchi.
Katika marekebisho hayo,
utatolewa msamaha kwenye mitambo (machinery) na vipuri vyake
vinavyotumika kwenye uchimbaji wa madini lakini hautahusisha vipuri vya
magari vitakavyoagizwa na makampuni yanayojihusisha na uchimbaji wa
madini.
Katika bajeti hiyo, pia umetolewa msamaha wa ushuru wa
forodha kwenye vyuma vinavyowekwa kwenye kingo za barabara na lengo lake
ni kutoa unafuu katika ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Alisema
ushuru wa forodha umepunguzwa kwa ving’amuzi kutoka asilimia 25 hadi
asilimia sifuri ili kuwezesha mabadiliko katika teknolojia ya analogia
na kwenda katika teknologia ya digitali.
Alisema katika Bajeti hiyo, pia ushuru wa ngano umeondolewa kuwa asilimia 0 badala ya asilimia 35
Alisema
Serikali pia imesamehe VAT katika mashine za kutolea stakabadhi
(electronic fiscal devices), ili kupunguza bei yake na kuwezesha
wafanyabiashara wengi kuwa nazo, kuhamasisha matumizi yake na hivyo,
kuongeza mapato ya Serikali.
Katika eneo hilo, Serikali imeondoa
VAT kwa vifaa mbalimbali vya kuhifadhia, kusafirisha na kusambaza gesi
asilia ili kuongeza matumizi ya nishati hiyo katika sekta mbalimbali za
kiuchumi, kwenye magari, majumbani na viwandani.
Kodi kwa wafanyabiashara
Wafanyabiashara
ambao mapato yao hayazidi Sh3,000,000 hawatalipa kodi kuanzia Julai
Mosi, mwaka huu. Dk Mgimwa alisema mpango huo umefanywa kulinda mapato
ya Serikali.
Kabla ya msamaha huo, wafanyabiashara hao ambao mapato yao hayazidi Sh3,000,000 walikuwa wanalipa Sh35,000.
Marekebisho
mengine ya kodi ya mapato ni kuwa wenye mapato kati ya Sh3 milioni
–Sh7.5 milioni watalipa Sh100,000 badala ya Sh95,000.
Malengo ya Bajeti
Waziri
Mgimwa alisema Bajeti hiyo imejielekeza katika Kukuza Pato la Taifa kwa
asilimia 6.8 mwaka 2012 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.4 mwaka
2011.
Malengo mengine ni kuimarisha miundombinu ya uchumi,
ikijumuisha umeme, barabara, reli na bandari, kuongeza upatikanaji wa
huduma za kifedha na kuongezeka kwa mapato ya ndani yatakayofikia uwiano
na Pato la Taifa wa asilimia 18 kwa mwaka 2012/13 kulinganisha na
mwelekeo wa asilimia 16.9 mwaka 2011/12.
Dk Mgimwa alitaja malengo
mengine kuwa ni pamoja na kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei ili urudi
kwenye viwango vya tarakimu moja na kuwa na kiwango tengemavu cha
ubadilishaji wa fedha kitakachotokana na mwenendo wa soko la fedha.
Malengo
mengine ni kukuza mikopo kwa sekta binafsi kwa kiwango cha asilimia 20
ya Pato la Taifa ifikapo mwishoni mwa Juni 2013, sambamba na jitihada za
kudhibiti mfumuko wa bei, kuboresha mazingira ya wafanyabiashara wadogo
na wa kati, kulinda na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta
za huduma za jamii, kuimarisha utawala bora na uwajibikaji na kujenga
uwezo wa nchi kukabiliana na misukosuko ya kiuchumi na kifedha pamoja na
kushiriki kwa ufanisi katika ushirikiano kikanda na kimataifa.
Matumizi ya Maendeleo
Kuhusu
matumizi ya maendeleo, Waziri Mgimwa alisema itazingatia vipaumbele vya
miundombinu ya umeme - mkazo ukiwa upatikanaji wake kwa kuongeza
uzalishaji, usafirishaji na usambazaji na jumla Sh498.9 bilioni
zimetengwa.
Serikali pia itatekeleza mradi wa ujenzi wa bomba la
gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa mkopo kutoka Benki ya Exim ya
China wenye thamani ya Dola za Marekani 1.2 milioni utakaosimamiwa na
TPDC.
Kuhusu usafirishaji na uchukuzi, alisema mkazo katika sekta
hiyo utakuwa ni kuimarisha reli ya kati ikijumuisha ukarabati wa injini
na mabehewa ya treni.
“Kwa upande wa barabara, miradi inayopewa
kipaumbele ni pamoja na barabara zenye kufungua fursa za kiuchumi.
Katika usafiri wa anga na majini, miradi itakayotekelezwa ni pamoja na
ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege na uendelezaji wa gati ya Ziwa
Tanganyika. Jumla ya Sh 1,382.9 bilioni zimetengwa katika eneo hili,”
alisema.
Kuhusu maji safi na salama, alisema lengo ni - kuongeza
upatikanaji wake mijini na vijijini na kwamba kiasi cha Sh568.8 bilioni
kimetengwa.
Kwa upande wa kilimo, uvuvi na ufugaji alisema katika
sekta hizo, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi itawekeza katika
kilimo cha mpunga na miwa katika mabonde makuu ya Wami, Ruvu, Kilombero
na Malagarasi pamoja na kuongeza tija na thamani, kubadilisha mfumo wa
kilimo na kukuza kilimo cha misitu.
Kuhusu kuongeza uzalishaji wa
mazao ya chakula pamoja na kuhakikisha uhakika wa chakula, Serikali
itaimarisha utekelezaji wa dhana ya Kilimo Kwanza kwa kuhakikisha nguzo
zake zote zinaendelea kuzingatiwa.
Alisema mikoa inatakiwa
kuendelea kutenga ardhi na vijiji kutakiwa kupima na kurasimisha ardhi
kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na wa nje na kwamba kiasi cha Sh192.2
bilioni kimetengwa katika eneo hilo.
Ikizungumzia maendeleo ya
viwanda, alisema Serikali inakusudia kuendeleza viwanda vinavyotumia
malighafi zinazopatikana nchini; viwanda vinavyoongeza thamani ya
madini; viwanda vikubwa vya saruji na viwanda vya eletroniki na Tehama
pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na kutenga maeneo maalumu ya
uwekezaji mijini na vijijini na kukuza ubia kati ya sekta ya umma na
sekta binafsi.