Pages

Friday, June 22, 2012

DIAMOND AZUA GUMZO



Naseeb Abdul ‘Diamond Platinumz’ akiwa na gari lake jipya la kifahari aina ya Toyota Land Cruiser Prado alilonunua kwa shilingi milioni sabini na tano.
Gari la zamani la Diamond aina ya Toyota Opa.
Na Shakoor Jongo
STAA wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond Platinumz’ amezidi kudhihirisha jeuri ya fedha baada ya hivi karibuni kununua gari la kifahari aina ya Toyota Land Cruiser Prado kwa shilingi Milioni sabini na tano (75,000,000) Amani lina ushahidi.

Staa huyo alinaswa hivi karibuni na mapaparazi wetu akiliegesha gari hilo nje ya mgahawa maarufu katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

GARI LAANZA KUZUA GUMZO
Akiwa ndani ya mgahawa huo, baadhi ya mashabiki wake walizua mjadala kama gari hilo ni lake huku wengine wakisema gari analomiliki msanii huyo ni Toyota Opa lenye thamani ya shilingi milioni saba (7,000,000) kwa kuagizia nje ya nchi.
Hata hivyo, wadau hao walishindwa kumuuuliza msanii huyo kama yeye ndiye mmiliki halali wa gari hilo lenye namba za ‘chesisi’ RZJ 1200017972.

DIAMOND ANASWA LAIVU
Juni 19, mwaka huu staa huyo alinaswa na paparazi wetu maeneo ya Mwenge, jijini Dar es Salaam akishuka kutoka kwenye ‘ndinga’ hiyo na ndipo alipobanwa kufunguka kuhusu gari hilo jipya.
Diamond: “Kwa kweli ngoma (gari) ni yangu. Nilinunua hili nikiamini linaweza kunisaidia kwenye ruti zangu.”
Amani: Umelinunua shilingi ngapi?”
Diamond: “Shilingi milioni sabini na tano pamoja na mambo yote ya ushuru.”

ANATAKA NAMBA ZA KISASA
Aidha, msanii huyo ambaye kwa sasa amepaa kwa kupata mafanikio kupitia shoo zake, alisema amechelewa kuweka namba za usajili kwa sababu anataka kubandika namba binafsi ambazo zitakuwa na jina la DIAMOND.
Alisema namba hizo ambazo serikali iliruhusu hivi karibuni, zitamgharimu shilingi za Kitanzania milioni tano (5,000,000).

UTAJIRI TAYARI
Mbali na kununua gari hilo, pia Diamond anamiliki gari aina ya Opa, anajenga nyumba mbili za kisasa na kuna ushahidi kuwa anaingiza kuanzia shilingi milioni 16 kwa wiki kupitia shoo zake.
Kwa mahesabu ya kawaida, kama staa huyo anaingiza kiasi hicho cha fedha kwa wiki, ni dhahiri anatumbukiza shilingi 2,285,714,28 kwa kila siku.
Kwa maana hiyo, Diamond anaingiza shilingi 95,238.095 kila dakika sitini au kwa kila saa moja.
Kipato hicho ni shoo tu, mbali na hizo msanii huyo ana tenda za makampuni mbalimbali ambapo hufanya matangazo na kuingiza kipato cha nguvu.
Diamond anaweza kuwa msanii wa kwanza wa kiume katika Bongo Fleva Tanzania (kama kuna mwingine ajitokeze na vielelezo) kumiliki gari la kifahari.