Pages

Friday, June 22, 2012

MKAKATI WA KULIPENDEZESHA TAIFA NA SANAA ZA NYUMBANI

Wajumbe waliohudhuria kikao hicho wakifuatilia mchango wa mmoja wa wajumbe kwa makini.
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Shirikisho la Sanaa za ufundi nchini liko mbioni kuzindua kampeni ambayo italenga kujenga msukumo wa kulipamba taifa na Sanaa mbalimbali nyumbani.

Akizungumza wiki hii kwenye kikao cha awali cha maandalizi ya kampeni hiyo kilichofanyika BASATA jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa baraza hilo Ghonche Materego alisema kuwa, lengo ni kuhakikisha maeneo ya miji, majiji, manispaa, ofisi, mahoteli na mazingira mbalimbali yanaona umuhimu wa kununua sanaa za nyumbani na kuzitumia kupamba.

“Hatujapamba kabisa kwa sanaa zetu, maeneo mengi ya miji, kuta za maofisi, nyumba zetu na kadhalika ni matupu. Ni wazi kunahitajika msukumo wa pekee katika kuhakikisha tunaipendezesha nchi yetu kila mahali na Sanaa mbalimbali” alisisitiza Materego.

Kwa mujibu wa Materego, Tanzania ni nchi iliyojaaliwa vipaji vingi na yenye historia ya pekee katika Sanaa za Ufundi hivyo ingetarajiwa sanaa hizo kupamba kwa wingi miji, fukwe, maofisi, shule, majumba, mahoteli na maeneo mbalimbali.

“Sasa kama wasanii tuingalie nchi yetu, tujiweke mbele katika kuangalia namna ya kuipamba kwa Sanaa zetu.Tukichelewa itapambwa na Sanaa za nje” aliongeza Materego.

Alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Ikulu na Rais Jakaya Kikwete kwa kutilia mkazo mapambo ya Sanaa za nyumbani na kutoa wito kwa ofisi zingine za umma kuiga mkakati huo kwani ni aibu kutumia sanaa za nje kupamba.

“Mara baada ya Rais Kikwete kuingia Ikulu kulifanyika ukarabati, maonesho ya Sanaa za ufundi yaliandaliwa ili kupata Sanaa za kuipamba Ikulu yetu, hili ni jambo la faraja kwamba, na sisi tuna pa kuanzia” alisema Materego.

Alitaja faida za kampeni ya kulipamba taifa na Sanaa za nyumbani kuwa ni pamoja na kutanua soko la kazi za wasanii, kulipendezesha taifa na kazi mbalimbali za mikono, kuwathamini wasanii na nyingine nyingi.

Nchi ya Tanzania ni miongoni mwa mataifa yanayovuma kwa Sanaa za Ufundi duniani kama michoro, vinyago, ususi na kadhalika lakini pamoja na utajiri huo bado Sanaa hizi hazijapewa nguvu kubwa ndani ya mipaka.