WAZIRI
Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe jana aliwasilisha bungeni bajeti
mbadala ya Kambi ya Upinzani kwa mwaka wa fedha 2012/2013, huku
akibainisha kasoro lukuki katika bajeti ya Serikali ilioyowasilishwa
Alhamisi iliyopita.Bajeti ya Zitto ilitanguliwa na hotuba ya Msemaji
Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Ofisi ya Rais – Mipango, Christina
Mughwai ambaye pia aliweka wazi kile alichokiita udhaifu wa Serikali
katika kuitekeleza mipango yake ya kiuchumi, hali ambayo inasababisha
umaskini kwa wananchi.
Hotuba
zote mbili, ya Zitto na Lissu, zilisema licha ya Serikali kutangaza
kwamba bajeti ya 2011/12 ilikuwa ya kupunguza makali ya maisha, hakukuwa
na nafuu yoyote kwa wananchi kwani maisha yameendelea kupanda.
Pamoja
na kupendekeza njia kadhaa za kupanua wigo wa mapato ya Serikali,
wapinzani wametaka kufanywa kwa ukaguzi wa deni la taifa, ili kubaini
chanzo cha Serikali kukopa na kuweka wazi jinsi fedha hizo zilivyotumika
hadi kufikia Sh22 trilioni.
Zitto
ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni katika hotuba yake
alisema mapato ya Serikali yanaweza kuongezwa kwa Sh2.885 trilioni,
hivyo kupunguza utegemezi wa mikopo ya kibiashara ambayo imekuwa
ikiligharimu taifa kiasi kikubwa cha fedha.
Vyanzo
vya kodi na kiasi cha fedha kwenye mabano alivyopendekeza ni
marekebisho ya kodi za misitu ikiwamo mkaa (Sh130.8 bilioni), Kupunguza
misamaha ya kodi, kuzuia ukwepaji kodi na udanganyifu wa biashara ya nje
(Sh742.74 bilioni), Mauzo ya hisa za Serikali (Sh415.55 bilioni),
Marekebisho ya kodi Sekta ya Madini na asilimia 25 ya Mauzo ya Madini
Nje (Sh578.36 bilioni) na Marekebisho ya Kodi na Usimamizi bora wa
Mapato Kampuni za Simu (Sh502.26 bilioni).
Mapendekezo
mengine ni Marekebisho ya Kodi ya Tozo ya Kuendeleza Stadi (Sh243.52
bilioni), mapato ya wanyamapori (Sh61.64 bilioni), kuondoa msamaha wa
ushuru wa mafuta kwa kampuni za madini (Sh44.9 bilioni), Usimamizi wa
mapato ya utalii (Sh51.75 bilioni), Kuimarisha biashara Afrika Mashariki
(Sh 114.15 bilioni).
Zitto
alisema kama wapinzani wangekuwa madarakani wangekusanya kiasi cha Sh15
bilioni sawa na ile ya Serikali, lakini tofauti ni hatua ya kutenga
asilimia 35 ya mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya
maendeleo na kupunguza utegemezi wa bajeti kutoka asilimia 42.37 za
Serikali hadi asilimia 21.3.
Deni la Taifa
Kuhusu
deni la Taifa, mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini (Chadema), alisema
Serikali haipaswi kuendelea kukopa, kwani taarifa rasmi za kibenki na
ukaguzi wa hesabu zinaonyesha kwamba deni hilo linakua kwa kasi tofauti
na maelezo ya Serikali kwamba linahimilika.
“Taarifa
ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonyesha kuwa Deni
la Taifa linazidi kuongezeka kwa asilimia 38 kutoka Sh10.5 trilioni
mwaka 2009/2010 hadi Sh14.4 trilioni 2010/2011. Kwa mujibu wa Waziri wa
Fedha, Deni la Taifa limefikia Sh20.3 trilioni mpaka ilipofika mwezi
Machi mwaka 2012,”alisema Zitto na kuongeza:
“Ukisoma
taarifa ya Mwezi wa Mei 2012 ya Benki Kuu ya Tanzania, Deni la Taifa
sasa limefikia Sh22 trillion. Suala hapa sio ustahmilivu wa Deni kama
inavyodai Serikali, bali ni kwamba tunakopa kufanyia nini?”
Alisema
hesabu za bajeti ya Serikali ya 2012/13 inayopendekezwa zinaonyesha
kwamba Serikali bado ina mpango wa kukopa kwa ajili ya kugharamia
matumizi ya kawaida ambayo hayazalishi wala kutozwa kodi.
“Hatutaki
mikopo kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya posho, kusafiri, magari n.k.
Tuchukue mikopo kuwekeza kwenye miradi itakayokuza uchumi na kuzalisha
kodi zaidi,” alisema.
Kuhusu
mfumuko wa bei, Zitto alikosoa hatua zinazopendekezwa na Serikali
kukabiliana nao, kwamba ni zile zilizoshindwa katika mwaka wa fedha
unaoishia Juni 30, mwaka huu. kutoka Mwananchi. www.mwananchi.com