Pages

Tuesday, July 10, 2012

CHADEMA wamjibu Dk. Nchimbi, wagoma kuhojiwa na Polisi



CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema hakiwezi kukubali viongozi wake wanaodaiwa kutishiwa maisha kuhojiwa na Jeshi la Polisi kama imevyoelekezwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi kwani hawana imani na Polisi. Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Peter Slaa alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari Makao Makuu ya chama hicho Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Akitoa tamko hilo ambalo limepitishwa na Kikao cha Kamati Kuu iliyokutana tangu juzi, Dk. Slaa amesema hawaoni sababu ya kuhojiwa na Jeshi la Polisi kwa kuwa wamewahi kuwapa taarifa nyingi za vitisho dhidi yao na hakuna hata moja imefanyiwa kazi.
“Hatuwezi kwenda Polisi kwa sababu tumekuwa tukipeleka mambo mengi ya vitisho lakini hayafanyiwi kazi…na hili tulisha waambia hatuendi kwao labda watukamate,” alisema Dk. Slaa akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema yeye mwenyewe licha ya kuwasilisha madai mbalimbali aliwahi kutegeshewa vinasa sauti na kutoa taarifa polisi lakini tangu wachukue vifaa hivyo hawajasema chochote hadi leo, jambo ambalo limewafanya waamini hata wakienda huko hakuna chochote kitafanyika.
Dk. Slaa alisema leo asubuhi alipigiwa simu na mmoja wa maofisa upelelezi kutoka Makao Makuu ya Polisi akiomba miadi ya kukutana naye, jambo ambalo amesema hayupo tayari kuhojiwa na wanausalama hao wa raia labda wamkamate.
Alisema tayari baadhi ya viongozi wa Serikali wameanza kuipuuza malalamiko yao dhidi ya vitisho wakidai huenda viongozi wa CHADEMA wanatafuta umaarufu wa kisiasa kwa kutoa taarifa hizo, kitendo ambacho amesema umaarufu wao hautatokana na viongozi wa Serikali au CCM bali ni kwa kazi wanazozifanya kwa wananchi.
Juzi Dk. Nchimbi alisema taarifa za kutishiwa maisha dhidi ya viongozi wa CHADEMA ni nzito hivyo haziwezi kupokelewa kirahisi Jeshi la Polisi linaanza kazi ya kuwahoji wahusika ili kulifanyia kazi jambo hilo. Alisema suala la usalama wa raia si hiyari bali ni la lazima hivyo hata kama wahusika hawataki lazima taratibu zifanywe kuhakikisha usalama kwa wahusika.

Wakati huo huo CHADEMA inaanza ziara ya Oparesheni Sangara ambayo itafanyika katika mikoa mitano ya Tanzania ikiwemo Dodoma, Morogoro, Iringa na Manyara. Akizungumzia ziara hiyo ambayo itashirikisha viongozi wa juu wa CHADEMA, Wabunge, Wajumbe pamoja na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali. Dk. Slaa amesema ni ziara ya kukiimarisha chama ikiwa ni pamoja na kuangalia mchakato wa uchaguzi wa chama hicho unaoendelea ngazi za chini.
Alisema katika ziara hiyo ambayo kauli mbiu yake ni “Hakuna Kunywa, Kula wala Kulala” inatarajiwa kuzunguka katika majimbo ya uchaguzi 44 ya mikoa hiyo, Kata 806 na vijiji 4,000. Ziara hiyo inatarajia kutumia siku 104.
Akifafanua zaidi kuhusiana na ziara hiyo amesema CHADEMA ni chama ambacho kinajitofautisha na vyama vingine katika utendaji wake na ndiyo maana wanaendelea kufanya ziara zao vijijini kuangalia maisha ya wananchi mpango ambao ni mpya.
“Kuna taarifa za baadhi ya watu wanabeza ziara zetu kwamba zinalenga posho…no CHADEMA hakuna posho, kwenye ziara zetu tunakula hadi kwa mama ntilie (chakula cha kawaida), tutaendelea kupiga kelele hadi pale haki za Watanzania zitakapokuwa zikipatikana bila vikwazo…tunapigania haki ya kila mmoja awe mwanafunzi, wafanyakazi, wakulima na hata madaktari,” alisema Dk. Slaa.