Pages

Thursday, July 19, 2012

Gari la Polisi labambwa na Nyara za serikali!


JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro, limekamata shehena ya meno ya tembo iliyokuwa ikisafirishwa kutoka mji wa Tarakea mpakani na Kenya kwenda mjini Moshi.

Shehena hiyo ilikuwa ikisafrishwa ndani ya gari aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T 557 BST linalodaiwa kumilikiwa na askari polisi wa kituo cha Tarakea, Koplo Phabian.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alikiri jana kukamatwa kwa shehena hiyo na kwamba watu wawili wanashikiliwa kwa kosa la kukutwa na nyara za serikali.

Kamanda Boaz alisema gari hilo baada ya kupekuliwa lilikutwa likiwa na vipande sita vya meno ya tembo, ingawa hakuweza kufafanua zaidi meno hayo yalikuwa yasafrishwe kwenda nchi gani.

Waliokamatwa kwa mujibu wa Kamanda Boaz ni Sharifa Athuman (35) ambaye ni Mtanzania  anayeishi eneo la Kimana nchini Kenya na Raphael Emmanuel (25) mkazi wa Magamba mkoani Tanga.

Kwa mujibu wa kamanda, gari hilo lilikamatwa jana saa 2 asubuhi na askari polisi waliokuwa kwenye kizuizi cha barabara katika mji mdogo wa Himo Wilaya ya Moshi Vijijini.

Kukamatwa kwa meno hayo ya tembo kunakuja siku chache baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki, kukiri kuwapo na mtandao mkubwa wa majangili wanaojihusisha na biashara ya meno ya tembo na pembe za ndovu.

Kagasheki alikiri kuwapo kwa mtandao huo wenye nguvu  kifedha wakati akipokea faru watatu weusi kutoka nchini Uingereza, ambao walipelekwa katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.


Tanzania Daima