Pages

Thursday, July 26, 2012

Upelelezi wa kesi dhidi Mulundi, aliyemteka Dkt. Ulimboka Steven bado haujakamilika

Kesi ya kumteka na kutaka kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dkt. Steven Ulimboka inayomkabili raia wa Kenya, Joshua Mulundi (21), katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imetajwa na upelelezi wake haujakamilika.

Kesi hiyo imetajwa mbele ya Hakimu Agnes Mchome na wakili wa serikali alikuwa Mwanaisha Komba ambapo aliieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi haujakamilika. Kesi imepangwa kutajwa tena Agosti 8 mwaka huu.

Mulundi ambaye ni mkazi wa Murang’a , Kenya, anadaiwa kuwa Juni 26 mwaka huu, akiwa eneo la klabu ya Leaders alimteka Dkt. Ulimboka. Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa Juni 26 mwaka huu, akiwa katika eneo la Msitu wa Mwabepande Tegeta, Dar es Salaam, kinyume cha sheria, mshitakiwa huyo alijaribu kumsababishia kifo Dkt. Ulimboka.

Mshitakiwa alikana mashitaka hayo na yupo rumande.

via HabariLeo