Pages

Sunday, July 8, 2012

Viongozi wa dini wajitosa sakata la Dk Ulimboka


Viongozi wa madhehebu ya Kikristo na Kiislamu,wakiomwombea mwenyekiti wa Kamati ya Madaktari Dk. Stephen Ulimboka, baada ya kumalizika kwa mkutano huo, uliohudhuriwa pia na Viongozi wa Madaktari pamoja na Kamati ya madaktari uliofanyika Dar es Salaam jana.
Geofrey Nyang’oro na Aidan Mhando
VIONGOZI wa dini za Kikristo na Kiislamu wamejitosa katika sakata la Dk Steven Ulimboka ambaye yuko nchini Afrika Kusini kwa matibabu baada ya kutekwa na kupigwa na watu wasiojulikana pamoja na mgomo wa madaktari kwa kufanya mkutano na viongozi wa Jumuiya ya madaktari na wanaharakati jijini Dar es Salaam jana.Viongozi hao walipendekeza iundwe kamati huru ya kuchunguza tukio la kupigwa Dk Ulimboka mapema iwezekanavyo ili kupata ukweli wa kilichotokea.
Pia viongozi hao walishauri kuwa Rais Kikwete akutane na madaktari pamoja na viongozi wa dini ili kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wao unaoendelea nchini hivi sasa.Viongozi hao pia wameitaka Serikali kutoa ulinzi kwa Dk Ulimboka na madaktari wote wengine ili kuwahakikishia usalama wa maisha yao.
Akisoma tamko la viongozi hao, Mkurugenzi wa Baraza la Habari la Kiislamu(Bahakita), Hussein Msopa kwa niaba ya viongozi hao alisema kwamba, kuundwa kwa kamati huru ya uchunguzi  itasaidia kupata ukweli wa tukio la kutekwa na kupigwa kwa Dk Ulimboka na kuwezesha  kubaini wahusika wa tukio hilo.
“Tukio la kutekwa, kuteswa na kutupwa katika Msitu wa Pande Dk Ulimboka ni la kusikitisha… na tunamuomba Rais Kikwete aunde tume huru itakayojumuisha madaktari wenyewe, viongozi wa dini, wanaharakati na wanasheria kubaini kiini cha tatizo hilo.” alisema Msopa.
Kauli ya viongozi hao wa dini ni ya kwanza kutolewa kwa pamoja tangu kutokea kwa tukio la kutekwa, kupigwa na kutupwa kwa Dk Ulimboka katika Msitu wa Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Viongozi hao pamoja na kudai tume huru pia waliomba Serikali kufuta kesi  iliyofungua dhidi ya madaktari waliofukuzwa kutokana na mgomo na  kuwarejesha kazini ili  kumaliza mgomo huo waliodai unaathiri afya za Watanzania.
Tamko hilo limekuja siku chache tangu Serikali  ilipofungua kesi dhidi ya madaktari waliogoma kwa Baraza la Madaktari Tanzania ikilitaka kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki kwa madaktari hao.
Msopa alitaja sababu ya viongozi hao kuungana na wanaharakati kutafuta suluhisho la mgomo huo kuwa ni kuona Watanzania wanazidi kuteseka kwa kukosa huduma za matibabu.
“Tunafahamu kwamba, Rais Kikwete ameweza kutatua migogoro mingi mfano mgogoro wa Chadema, suala la Katiba Mpya, migogoro ya Zanzibar, hivyo pia sasa tunaamini katika hili la madaktari ataweza kulitafutia ufumbuzi,” alisema Msopa.
Kwa upande wake Mchungaji Lawrance Mzava wa Kanisa la Kiinjili la Assemblies of God (EAGT) Ubungo ambaye ni mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, alisema hiyo itakuwa njia sahihi ya kumaliza mgogoro huo unaotikisa nchi kwa sasa.
“Njia sahihi ya kuondoa mgogoro huo ni kufanya mazungumzo ambayo yatasaidia kufikia makubaliano yatakayoleta  ufumbuzi wa kudumu  wa mgomo wa madaktari,” alisema Mzava na kuongeza:
“Sisi  tunaamini kuwa njia sahihi ya kuleta  suluhu ya mgogoro huu ni kwa Rais  Kikwete kukutana na  kufanya  mazungumzo na sisi (viongozi wa dini) na madaktari,” alisema.
Mgomo
Mgomo wa madaktari unaoelezwa kumalizika kwa kusuasua ulianza Juni 23 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Mifupa (MOI) na kusambaa hospitali mbalimbali nchini, madaktari wakitoa madai mbalimbali kuitaka Serikali iyatekeleze.

Hata hivyo, hadi jana upatikanaji wa huduma MNH  na Taasisi ya Mifupa (MOI), umezidi kuzorota, huku baadhi ya madaktari wakisema tukio la Dk Ulimboka limewapunguzia ari ya kufanya kazi.

Wakizungumza  kwa sharti la kutotajwa majina, baadhi ya madaktari wa MNH, walisema tukio la kutekwa, kupigwa na kutupwa kwa Dk Ulimboka  limewatisha.

“Kwa sasa madaktari hawana ari, hata wakifika eneo la kazi bado suala la kufanya kazi ni kitu kingine, lakini kitendo cha kutekwa kwa Dk Ulimboka kimetutisha sana, ” alisema mmoja wa madaktari hao wa MNH.

Uchunguzi wa gazeti hili  umebaini kuwapo kwa baadhi ya madaktari bingwa katika MNH pamoja na MOI, ambao nao walithibitisha kuwa utendaji kazi hauwezi kuwa wa ufanisi kwa njia ya kulazimishwa.

“Serikali inachotakiwa siyo kulazimisha, inapaswa kusikiliza na kutatua hoja, sisi madai yetu yamepotoshwa, hatuna vifaa vya kufanyia kazi, lakini wananchi hilo hawalielewi,” alisema mmoja wa madaktari hao.

Hata hivyo, Msemaji wa MNH, Eminael Aligaesha alisisitiza kuwa huduma katika hospitali hiyo zinarejea hatua kwa hatua.

“Unajua tulikuwa katika kipindi kigumu lakini, niseme tu huduma zinazidi kuimarika siku hadi siku,” alisema Aligaesha.

Juzi Serikali iliwaandikia barua za kuwashtaki madaktari wote waliofukuzwa kazi kutokana na mgomo huo kwa Baraza la Madaktari Tanzania.

Katika barua hizo ambazo habari zinadai  wamekabidhiwa madaktari waliofukuzwa kutokana na mgomo, Serikali  kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imelitaka baraza hilo kuchunguza na kuchukua hatua dhidi yao.

Baraza la Madaktari Tanzania ndilo lenye dhamana ya kusajili madaktari na ndilo lenye uwezo wa kutoa adhabu kwa madaktari hao ikiwa ni pamoja na kufuta usajili dhidi yao.

Sehemu ya barua hizo iliyosainiwa na T.A. Chando kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara ya hiyo inasomeka; “Daktari mtajwa hapo juu alipelekwa katika Hospitali ya Taifa (MNH) kufanya mazoezi ya kuboresha taaluma kwa vitendo, tumepokea malalamiko kuwa kati ya Juni 23 na 29 mwaka huu alikataa kutoa huduma za kitaalamu ikiwa ni wajibu wake kama Daktari.

“Kitendo hicho siyo tu kilihatarisha usalama wa wagonjwa walioletwa katika hospitali hiyo kwa matibabu, bali pia ni kinyume na maadili ya taaluma ya udaktari.”