Elias Msuya
SINA lengo la kujadili kauli ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika aliyoitoa hivi karibuni na kusababisha kufukuzwa kwenye kikao cha Bunge kwa kukiuka kanuni.
Lakini nimedhamiria kujadili udhaifu wa Serikali unaosababisha maisha ya Watanzania kuwa magumu. Tanzania siyo masikini lakini wananchi wake ni masikini wa kutupwa. Wafanyakazi wanagoma, wananchi wengine wanalia hali ngumu.
Ni mara ya pili sasa tunashuhudia mgomo wa madaktari nchini. Pamoja na utetezi mwingi wa Serikali, bado ukweli unabaki kwamba Serikali imeshindwa kutimiza wajibu wake ndiyo maana watumishi hao wameamua kuchukua hatua hiyo.
Mgomo wa kwanza wa madaktari uliosababisha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Blandina Nyoni na aliyekuwa Mganga mkuu wa Serikali Deo Mtasiwa kusimamishwa kazi kwaajili ya uchunguzi, ulimalizika kwa ahadi ya Serikali kushughulikia madai hayo.
Serikali iliunda kamati ya kushughulikia madai hayo baada ya wawakilishi wa madaktari kwenda Ikulu kumwona Rais Jakaya Kikwete ikiwa ni siku chache tu tangu walipokutana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Leo miezi mitatu imepita, Serikali bado inarudi na hadithi zilezile za kuwataka watumishi hao warudi kwenye mazungumzo yasiyo na kikomo.
Wakati madaktari wakendelea na mgomo wao, walimu nao wanawasha indiketa kwamba wako mbioni kugoma.
Walimu wamekuwa na madai mengi kwa muda mrefu. Kwanza wanalipwa mshahara mdogo, vilevile wanaidai Serikali malimbikizo ya fedha za kujikimu, posho za muda wa ziada na nyinginezo.
Haya yote yameimbwa kwa muda mrefu, lakini Serikali imelala fofofo. Sasa kwa kuwa walimu wametangaza kugoma, ndiyo Serikali inaamka usingizini.
Sikubaliani na utetezi wa Serikali kwamba haina fedha za kutosha kutekeleza madai hayo. Fedha zipo, tatizo haijulikani zitumikeje.
Kuna matumizi makubwa ya Serikali yanayogharimu fedha nyingi na yamesemwa sana. Kwa mfano ukubwa wa baraza la mawaziri, hauna manufaa yoyote zaidi ya kubebana tu. Nchi ingetosha kabisa kuwa na mawaziri hata 25 tu na ikaenda. Wizara nyingine zinapaswa kuwa idaratu za Serikali.
Ukubwa huo wa Serikali unasababisha kuwepo kwa matumizi makubwa ya fedha ikiwa ni pamoja na usafiri unaohusisha magari ya kifahari, nyumba, mishahara na marupurupu ya kila aina.
Hayo yote yanaliwa na kundi la viongozi wa Serikali huku watumishi wengi wa Serikali wakiumiza vichwa hata kupata mshahara wa mwezi.
Serikali imebaki kuwapiga chenga watumishi wake kila kukicha, matokeo yake sasa wanaona njia nzuri ni kugoma na kuandamana. Huu ni udhaifu mkubwa wa Serikali.
Mambo mengine hayahitaji hata kutumia fedha. Kwa mfano, baada ya mgomo wa kwanza wa madaktari, ndiyo Serikali ikaona kwamba Katibu wa Wizara ya afya na mganga mkuu wana hatia, wakasimamishwa. Kwa maana nyingine kama siyo mgomo ule wangekuwa wanadunda hadi leo.
Kwa maana hiyo pia Serikali huenda imejaza watendaji wabovu, lakini kwakuwa hakuna migomo, basi wanaendelea kula na kunywa kodi ya wananchi.
Huo ndiyo udhaifu mkubwa wa Serikali yetu, hatuna viongozi wawajibikaji, badala yake wanasubiri kushtuliwa na migomo.
Udhaifu mwingine ambao hata Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuusema ni Serikali kushindwa kukusanya kodi.
Tumeshuhudia bajeti ya mwaka huu ambayo imeendelea kutegemea mapato ya ndani kutoka kwenye vitu vidogo vidogo kama vile pombe, sigara, juisi huku ikiwaachia wawekezaji wakubwa wa kigeni rasilimali kubwa kama madini, misitu, ardhi wanyamapori na nyinginezo.
Wawekezaji hao sasa wamekuwa watawala tena hawana tofauti na wakoloni waliowatawala mababu zetu huko nyuma kwani Serikali inmatoa misamaha mikubwa ya madeni kwao.
Huu ni udhaifu mkubwa na ndiyo umeifikisha Tanzania hapo ilipo. Leo Watanzania ni masikini siyo kwa sababu nchi ni masikini, bali Serikali ni dhaifu, haikusanyi kodi.
Afadhali Mwalimu Nyerere ambaye aliamua kutaifisha rasilimali zote na kuziweka mikononi mwa Serikali. Hata kama mashirika yaliyotaifishwa yalikufa, lakini angalau alionyesha jeuri ya kujitegemea.
Leo viongozi wetu hawana jeuri hiyo, wamegawa kila kitu kwa ‘wawekezaji’, hata kodi wanaogoma kuwatoza.
Ndiyo maana Serikali naina fedha za kutosha kuwahudumia watumishi wake. Watumishi hao wamekuwa omba omba na wakopaji wakubwa kwenye vyombo vya fedha. Hata ufanisi wa kazi haupo kwa sababu wengi wanafikiria kulipa madeni.
Afadhali basi wana uwezo hata wa kugoma, lakini tukumbuke kuna kundi la wananchi wasio na ajira kama vile wamachinga, wakulima, wavuvi na wengineo. Hao wanaishi kwa kudra za Mwenyezi Mungu. Hawana haki hata kwenye ardhi wanaoishi, kwani siku akitokea mwekezaji na kuitaka ardhi yao, wanafukuzwa tu.
Sina lengo la kuibeza Serikali yetu, lakini hapo ndipo Watanzania tulipofikishwa. Jambo la msingi ni viongozi wa Serikali kukubali ukweli kwamba Serikali ni hdaifu na wabadilike. Wawe wakali kwa mchwa wanaotafuna mali za umma.
Elias Msuya ni mwandishi wa makala wa gazeti la Mwananchi; 0754 897 287