Lauden Mwambona
NYUMBA 300 zilizojengwa na Mfuko wa Hifadhi ya
Jamii (NSSF) eneo la Kijichi Dar es Salaam zitauzwa kati ya Sh60milioni
na Sh120 milioni, ilifahamika mwishoni mwa wiki.Maofisa wa NSSF
walisema hayo walipotoa taarifa za kazi mbalimbali za mfuko kwa watu
waliotembelea banda lao kwenye Maonyesho ya Biashara yaliyofikia kilele
juzi kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere jijini hapa.
Ofisa
Uwekezaji Mkuu wa NSSF, Gerald Sondo alisema ujenzi wa nyumba hizo
zinazotofautiana kwa idadi ya vyumba umekamilika na kwamba hivi sasa
wanaendelea na kazi za kuweka umeme, kupeleka maji na kutengeneza
barabara.
Sondo alisema uuzwaji wa nyumba hizo utafanywa na Benki
ya Commercial Bank Of Africa (CBA) na kwamba benki hiyo imeelekezwa
kuwafikiria zaidi wanachama wa NSSF.
“NSSF imeingia makubaliano
na CBA itakayowauzia kwa fedha taslimu au kuwakopesha Watanzania hususan
wanachama wa NSSF nyumba zilizoko Kijichi wilayani Temeke . Utaratibu
wa malipo ni papo kwa papo au kukopesha kwa kipindi kisichozidi miaka
15’’ alisema.
Naye Ofisa Mwekezaji wa mfuko huo, Sakina Mbiru
alifafanua kwamba kinachotakiwa sasa kwa watu wanaotaka nyumba ni
kufungua akaunti kwenye benki hiyo ili kujiweka kwenye mazingira mazuri
ya kufikiriwa kwanza.
Alipoulizwa juu ya kuwapo kwa riba kubwa
kupitia benki hiyo, alisema NSSF na benki hiyo wamekubaliana kutoa riba
ndogo zaidi kwa mikopo ya nyumba hizo na kwamba bei ya nyumba hizo
imezingatia ubora na thamani ya ardhi Dar es Salaam.
Wakati
huohuo, NSSF hatimaye itaanza kufunga mitambo ya ATM jijini Dar es
Salaam na mikoani mwishoni mwa mwezi huu ili kuwarahisishia wanachama
wake kujua michango na mambo mengine muhimu.
Ofisa Mwendeshaji
wa mitambo ya kompyuta wa NSSF, Kassim Mwandoro alisema kwa sasa
wamepata ATM 10 na kwamba lengo ni kuzifunga kwenye maeneo yenye
wanachama wengi na maeneo ya mbali hususan migodini ambako kuna
wanachama wengi pia.
NSSF ilizindua mpango wake wa Smart Card
miaka 10 iliyoita, lakini utekelezaji wake ulikuwa ukisuasua kutokana na
sababu ambazo hazikuwa wazi kwa wanachama wengi