Na: Maggid Mjengwa,
WATANZANIA tumekumbwa tena na balaa la ajali kubwa ya meli kuzama. Ni
wakati sasa wa kujifunza kutokana na yaliyotokea huko nyuma.
Maana ajali ya Mv Skagit inaonekana dhahiri kuchangiwa na uzembe. Na
uzembe kwa nchi yetu unalelewa na mfumo mbovu. Na mfumo mbovu unatokana
na Katiba mbovu.
Maana, ni katika mazingira haya ya kufanya mambo ya hovyohovyo ndipo
tunapokuwa na wanasiasa wa hovyohovyo wenye kuhusika pia na biashara ya
uchukuzi na usafirishaji wa abiria.
Ni vigumu kwa mfumo wetu wa sasa, kwa watendaji wa vyombo au taasisi
zisizo huru kikatiba na kisheria kuweza kuwasimamia wafanyabiashara
dhalimu ambao miongoni mwao wamo baadhi ya wanasiasa wetu.
Tuna lazima sasa kupitia Katiba yetu ijayo, kuvipa nguvu za kisheria
vyombo na taasisi zetu muhimu kwa nchi yetu. Tuwe na vyombo na taasisi
huru ambazo utendaji wake hauwezi kuingiliwa kirahisi na mamlaka
nyingine.
Fikiri leo kama tungekuwa na utaratibu wa kwamba mmiliki wa chombo cha
majini au angani na atakayebainika kuingiza nchini chombo kilicho chini
ya viwango vinavyokubalika kimataifa na hata chombo hicho kikasababisha
ajali ya kuua raia kuwa mmiliki huyo atafungwa jela na kufilisiwa mali
zake? Naamini, tungekuwa na vyombo madhubuti na ajali zingetokea kwa
bahati mbaya kwa maana yake halisi.
Ni nini basi cha kujifunza kutoka kwenye ajali iliyopita ya Mv Spice Islanders?
Ikumbukwe, Ripoti ya Tume ya kuchunguza ajali ya kuzama kwa Meli ya Mv
Spice Islanders ilipendekeza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari,
Mustafa Aboud Jumbe pamoja na wahusika wengine wachukuliwe hatua za
kisheria na kinidhamu kutokana na uzembe waliofanya na kusababisha
kuzama kwa Meli hiyo. Mpaka leo hii hatujasikia adhabu walizopewa wahusika wa ajali ile.
Maana, bado tunakumbuka kuwa, ripoti ile ilibainisha kuwa miongoni mwa
watu ambao walibainika na makosa katika ajali ya Mv Spice Islanders ni
pamoja na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar, Haji
Vuai Ussi, Mkuu wa kituo cha usimamizi wa usalama wa vyombo vya baharini
wa Shirika la Bandari, Usawa Khamis Said na Kaimu Mdhibiti wa Bandari
ya Malindi, Sarboko Makarani Sarboko.
Wengine ni pamoja na Wanahisa wa Kampuni inayomiliki meli hiyo Jaku
Hashim Ayub ambaye ni Mwakilishi na Mbuge wa Jimbo la Muyuni, Salim Said
Mohammed, Makame Hasnuu Makame na Yussuf Suleiman Issa.
Alikuwamo pia nahodha wa meli Said Abdallah Kinyanyite na wasaidizi
wake, Ofisa usafirishaji wa Shirika la Bandari Hassan Mussa Mwinyi na
Mkaguzi wa Meli wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini, Juma Seif Juma.
Ndiyo, wakati bado hatuna hakika ya hatua zipi zilichukuliwa dhidi ya wahusika hawa leo tunaomboleza msiba mwingine kwa taifa.
Hakika, inasikitisha sana, kuwa hata mwaka haujatimu kukumbuka ajali
iliyopita ya Septemba 9, 2011, Watanzania tunapatwa na msiba mwingine.
Na misiba yote miwili inatokana na uzembe na wala si ya kusingizia ‘Kazi
ya Mungu’.
Watanzania sasa tunataka kuona hatua kali za kisheria na kinidhamu
zinachukuliwa, tena kwa haraka dhidi ya wahusika waliochangia kwenye
ajali ile ya Mv Skagit.
Kwa kuanzia jina la mmiliki wa meli liwekwe hadharani. Na Tume
itakayochunguza ajali hii itabaini kuwa mwenye meli ameingiza chombo
chakavu, basi, awe wa kwanza kutolewa mfano.
Maana, kama taifa, bila kuwa wakali katika haya ya msingi, basi, tunahatarisha usalama wa taifa letu pia. Kamwe tusiruhusu hilo kutokea. Nahitimisha.
http://www.mjengwablog.com/