Pages

Tuesday, July 31, 2012

Manispaa ya Kinondoni itaanzisha wodi za matibabu ya kulipia

Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, imejipanga kuazisha wodi za kisasa za kulipia 'Fast track', katika Hospitali ya Mwananyamala ambazo zitatoa huduma bora kwa wananchi.

Naibu Meya wa Manispaa hiyo, Bw. Songoro Mnyonge, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akitoa ufafanuzi juu ya hatua walizo zichukuwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za matibabu katika hospitali hiyo, “Tunaamini mwaka huu wa fedha, tutaanzisha huduma hii katika Hospitali ya Mwananyamala, ingawa watalipia lakini mgonjwa atajisikia faraja zaidi kupata huduma bora kwa gharama ndogo, hadi sasa tuna wataalamu wa kutosha,” alisema.

Alisema kwa kuanzia, watakuwa na wodi ya wanawake, wanaume na wataanza kuchukua wagonjwa ambao ni wanachama wa Bima za Afya na baadae wanatarajia kuwa na wodi ya watoto, “Tumeamua kuanzisha huduma ya matibabu ya kulipia kwa sababu baadhi ya Watanzania hawana utamaduni wa kwenda kutibiwa katika hospitali za umma,” alisema.

Alitoa wito kwa wananchi kuwa na tabia ya kwenda kuhudumiwa katika hospitali za umma ambazo zina usalama mkubwa kwa afya zao na wataalamu wazuri.

Darlin Said