Wednesday, August 8, 2012

Makala: Wasanii wakongwe onesheni ukongwe wenu na sio kulaumu mnabaniwa


Makala: Wasanii wakongwe onesheni ukongwe wenu na sio kulaumu mnabaniwa

Profesa Jay

Na Emmanuel Msigwa aka DJ Msigwa, Radio Journalist, Radio DJ, Presenter & Club DJ


Neno mkongwe lina maana kubwa sana na kila mwenye kuitwa jina hilo anabeba uzito Fulani, iwe katika nyanja ya kisiasa,uchumi & sanaa na hata michezo. Mtu huyo hutegemewa kufanya kitu kizuri katika eneo lake husika ili liwe mfano kwa vijana wanaotamani kuwa kama yeye. Mathalani mchezaji wa mpira wa miguu wa timu ya taifa ya Italia aitwaye Andrew Pirlo, tumeona jinsi alivyotumia kipaji chake na hasa kuonyesha ukongwe wake katika timu wakati wa michuano Euro iliyomalizika hivi karibuni katika nchi za Poland & Ukrane ambazo ndizo zilikuwa wenyeji wa michuano hiyo,kiasi kwamba kila mmoja wetu amekuwa akilitaja jina lake. Utasikia mtu wa mpira akisema “ Pirlo bwana yule mzee fundi sana” hapa utaona jina mzee limetumika kama mkongwe!
Lady Jaydee
Njoo katika tasnia ya muziki ambako ndiko nilikokusudia kuyaandika haya utakayoyasoma. Hakika nchi yetu imejaliwa sana katika tasnia ya muziki kuanzia ule wa dansi mpaka wa muziki wa kizazi kipya na tunajivunia kuwa na wakongwe katika kila idara. Lakini je, ukongwe wa watu hawa unaleta tija? Unatoa mwangaza kwa vijana chipukizi? Unaonyesha kweli ukomavu wao? Je wanaweza kweli kuwanyooshea vijana hao chipukizi vidole kuwa eneo fulani wanakosea ilhali wao wenyewe wanakosea? Hawawezi kufanya hivyo kwa sababu wao wenyewe hawaonyeshi ukongwe wao. Hatuoni ukomavu wao ambao tunatarajia tuuone!

Unapotaja wakongwe ambao wapo katika tasnia ya muziki wetu wa kizazi kipya hautakosa kuwataja watu kama Mr II,Lady JD,Prof Jay nk hawa ni watu ambao wamehangaika na muziki huu kuufikisha hapa ulipofikia hakuna ambaye hajui juhudi zao.Hakuna ambaye havijui vipaji vyao. Sote tunakubali kwamba hawa ni majabari ya muziki wa kizazi kipya. Kwangu mimi hilo sina tatizo nalo japo lipo tatizo ambalo mimi  ninaliona na ndilo lilonisukuma kuandika makala hii. Makosa yanayofanywa na wasanii wetu wakongwe! Licha ya ukongwe wao lakini yapo makosa ambayo yanawarudisha nyuma, makosa hayo huwapa chipukizi nafasi za kutokea!

Juma Nature
Mathalani mkongwe Profesa Jay zamani kama Niggar Jay, kwa siku za karibuni naona jamaa kama anatoka nje ya mstari, kwa nini? Nitakwambia na kama nikikosea niambie! Hakuna ambaye hajui uwezo wa huyu jamaa katika kuandika mashairi makali ya hip hop. Ni mmoja kati ya ma legendary wa muziki wetu wa kizazi kipya lakini jamaa anaangushwa sana na kazi zake za video nitakupa mfano, unamfahamu Ryan Leslie? Kama haumfahamu ngoja nikufahamishe machache kuhusu yeye, jamaa ni mwandishi wa nyimbo,mtayarishaji wa nyimbo “ producer” na pia ni mwimbaji, je umekwisha wahi kuangalia baadhi ya nyimbo zake? Unaufahamu wimbo wake unaitwa BEAUTIFUL LIE? Je umekwisha angalia video yake? Kama bado tafuta na uangalie!

Wapo wasanii wakongwe Marekani mmoja wao ni Dr Dre, jamaa kwa ukongwe wake kila anachokifanya  unaona kabisa ukongwe wake unaleta somo kwa vijana chipukizi wa kimarekani. Mbona wakongwe wetu hatuoni ukongwe wenu? Umewahi kusikiliza  toleo jipya la wimbo wa Profesa Jay unaitwa Kamili Gado kamshirikisha  produza Marco Chali? ( ni toleo lake jipya kwa kuwa hana wimbo mpya tofauti na huo) Je umewahi kuangalia video yake? Je inaendana na ukongwe wa jamaa? Ki ukweli HAPANA! Na hapo ndipo makosa wanayofanya wakongwe wetu yanapoonekana.Kwa nini wasanii chipukizi wasiwapige bao? 
Afande Sele
Kama wewe ni mkongwe ambaye tunakutegemea kwanini uuchezee ukongwe wako? Kitu gani ambacho Jay anaweza kukisifia katika video hiyo? Rangi sawa,wale wasichana sawa, uchanganyaji wa picha nao sawa? Vipi kuhusu story board yake mbona ni wimbo ambao unauona kabisa mwenekano wake?
Kama mnaona ni ngumu kutengeneza “kichupa bora” ni bora msiwe mnatoa video ambazo zitashusha thamani ya ukongwe wenu.

Ninyi ni watu tunaowatagemea vijana wajifunze kufanya kilicho bora kutoka kwenu ama sivyo vijana hao watakuwa wanawapiga bao nanyi mnabaki kulia kuwa media zinawabania wakongwe, si kweli, ni ubora wa kazi zenu ndiyo utakaowaokoa iwe audio au video zenu. Kama hazitakuwa bora hakuna atakayewabeba!
Gangwe Mob
Kwa sasa vipindi  vya redio au runinga hakuna anayetaka viwe  vibaya ni lazima viwe  vizuri kwa maana ya kujipatia wasikilizaji au watazamaji, kazi nzuri haiitaji kujua ni mkongwe au chipukizi kafanya, kazi nzuri ni nzuri tu! Badilikeni wakongwe wetu. Fanyeni kazi zenye kiwango kikubwa kulinda ukongwe wenu utakaowafanya muendelee kupendwa daima. Watanzania wana hulka ya kupenda kilicho bora pasipo kujali aliyefanya hivyo ni mkongwe ama la!
Onyesheni ukongwe wenu, teteeni nafasi zenu ili tujivunie ninyi na tuweze kuwanyooshea vidole vijana chipukizi kwa kutoa mifano yenu na wao naamini watakubaliana na sisi na muziki wetu uzidi kuvuka boda hadi boda mkiamua mnaweza sana na nafasi mnayo……………………..kazi kwenu!

Thanx www.leotainment.blogspot.com