Benjamin Masese na Christina Gauluhanga, Dar es Salaam
MAMLAKA
ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeongeza muda wa wiki moja kwa wakazi
wa Dar es Salaam wenye sifa ya kupatiwa vitambulisho hivyo.
Taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana na Mkurugenzi wa NIDA, Dickson Maimu alisema shughuli hiyo itamalizika Agosti 6, 2012 huku akisisitiza muda mwingine hautaongezwa tena.
Maimu alisema wageni wote wanapaswa kujaza fomu 2A kwa kueleza ukweli uraia wa nchi zao na hadhi ya ukaazi wao.
Alisema
kwa mujibu wa sheria za usajili na utambuzi wa watu kifungu cha 9 (2)
waombaji wasiojua kusoma na kuandika watasaidiwa kujaziwa fomu na wale
wanaojua kusoma na kuandika watapewa fomu ili kujaza wenyewe chini ya
usimamizi wa usajili wa kituo husika.
Maimu
alisema kwa mujibu wa kifungu cha 20 (1) C inaeleza kwamba ni kosa la
jinai kutoa taarifa ambazo si sahihi zikiwamo za uraia na kuongeza
atakayebainika atatozwa faini au kwenda jela miaka isiyozidi mitatu.
Vile
vile alisema watu walio katika makundi maalumu kama wazee, walemavu na
wagonjwa watapelekewa mahitaji yao pale walipo na viongozi wa Serikali
za mitaa.
AWALI
kabla ya kuongezwa kwa muda huo shughuli hiyo ilikuwa imeonekana
kukwama kutokana na kujitokeza kasoro kadhaa zilizosababisha baadhi ya
wananchi kushindwa kujiandikisha.
Wakizungumza
jana na MTANZANIA kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi waliojitokeza
kujiandikisha katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam, wamesema
NIDA haikuweka utaratibu mzuri jambo ambalo linaonekana kusababisha
wananchi kukosa haki ya kujiandikisha kwa siku zilizopangwa.
Mkazi
mmoja wa Mongola la Ndege, Herbert Masamu amesema shughuli hiyo imekuwa
ngumu kutokana na uchache wa watu waliopangwa kuandikisha taarifa za
wananchi jambo ambalo limesababisha msongamano katika vituo mbalimbali.
Alisema
pia kukosekana kwa elimu ya kutosha za nyaraka au taarifa muhumi
anazotakiwa kuwa nazo mwananchi anayekwenda kujiandikisha nalo limekuwa
ni kero kwa wananchi hivyo kulazimika kwenda na kurudi katika vituo vya
kuandikisha bila kufanikiwa kujiandikisha.
“
Katika hili la uchache wa watu wanaoandikisha limetusababishia usumbufu
hivyo NIDA wanapaswa kuongeza siku na idadi ya waandikishaji kama
ilivyo kwenye kitambulisho cha kupigia kura ili kila mwananchi apate
haki ya kujiandikisha,”alisema Masamu.
Kiwalani
Katika
siku mbili za Jumamosi na Jumapili,MTANZANIA ilifanikiwa kufika katika
vituo mbalimbali kikiwamo cha Hali ya Hewa kilichopo kata ya Kiwalani na
kushuhudia umati wa watu wengi wakisubiri huduma hiyo bila mafanikio.
Katika
kituo ambacho hicho kinachounganisha zaidi ya mitaa mitatu, kulikuwa na
hali ya kushangaza kutokana na wananchi kufika kituoni kuanzia saa 12
alfajiri ili kuwahi kujipanga foleni huku wafanyakazi wa NIDA hawaoneki
kituoni.
Katika
kituo hicho, mwandishi wa gazeti hili alikuwa ni mmojwapo ya
wanaohitaji kuandikishwa lakini hakuweza kupata fursa kutokana na
waandikishaji kuchelewa kufika kituoni na kufanya kazi pole pole.
Hata
hivyo ilipofika saa 3.13 asubuhi alionekana Mwenyekiti wa Mtaa wa
Minazi Mirefu, Ubaya Chuma na kuanza kutoa maelekezo kwa wananchi
utaratibu uliopo .
Licha
ya kutolewa maelekezo hayo lakini wafanyakazi hao hawakutokea hadi
ilipofika saa 3 .27 asubuhi ndipo wandikishaji watatu walionekana hapo
na kuanza huduma huku mtu mmoja akichukua kati ya dakika 20 na 30
kuandikishwa.
Katika
kituo hicho cha Hali ya Hewa ilielezwa kwamba kuna waandikishaji 10
lakini hadi inafika saa 10 .03 walikuwa wamefika saba kitendo ambacho
kilisababisha ongezekao kubwa la wananchi huku wakilalamika.
Wakizungumza
na MTANZANIA baadhi ya wananchi walisema msongamano huo unasabishwa na
wafanyakazi wa NIDA kuchelewa kufika kituoni pamoja na utaratibu
uliowekwa.
Wananchi
hao walililamikia kituo kutokana na na kuwapo na matatizo mengi
yakiwamo kitabu kuibiwa cha orodha ya wananchi kitendo kilichomlazimu
Chuma kuweka utaratibu wa kuwatambua wananchi hao.
Vile
vile katika kituo hicho kuina wananchi walipatikana wakiwa na photocopy
ya kitambulisho cha kupigia kura cha mtu mwingine wakitaka kukitumia.
Kwa
mujibu wa Ubaya aliwaeleza wananchi hao kwamba kuna watu wachache wasio
wadilifu wanachukua kadi za kupigia kura za watu wengine na kubandua
picha za mtu halali na kubandika za kwao kisha kuzitoa photocopy.
Chanzo: Mtanzania