Saturday, June 30, 2012

DR. Ulimboka Ana Siri Nzito


ASEMA ATAANIKA KILA KITU BAADAYE, ASEMA ACHWE APUMZIKE, MKUU WA JOPO LA MADAKTARI WANAOMTIBU ASEMA ALING'OLEWA KUCHA, MENO MAWILI NA KUPATA MTIKISIKO WA UBONGO.

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari aliyetekwa nyara na kuumizwa vibaya usiku wa kumkia juzi, kisha kutupwa Msitu wa Pande, Dk Steven Ulimboka amesema atazungumza kwa kina yote yaliyomsibu baadaye na kuomba sasa aachwe auguze maumivu makali yanayomkabili.

Dk Ulimboka aliokotwa na wasamaria wema juzi asubuhi katika Msitu wa Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, baada ya kutekwa nyara na watu waliokuwa na silaha akiwa katika Viwanja vya Klabu ya Leaders, Kinondoni.

Jana, Dk Ulimboka ambaye amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili huku hali yake ikiwa haijatengemaa vyema, alitoa kauli akisema ingawa ana maumivu makali anaendelea vizuri ikilinganishwa na siku ya kwanza.

Dk Ulimboka alitoa kauli hiyo baada ya kutakiwa aeleze mkasa huo uliomfika wa kukamatwa, kuteswa na kutupwa msituni.
Hata hivyo, hadi sasa wingu zito la nani alimteka na watekaji walitaka kujua nini kutoka kwa kiongozi huyo wa madaktari, bado limetanda.

Siri nzito
Akisimulia mkasa huo kupitia Kituo cha Redio cha Clouds FM, Dk Ulimboka alisema, akiwa katika klabu hiyo ya Leaders alipigiwa simu na rafiki yake ambaye alikuwa atokee Tandika na baada ya kumsubiri ndipo alipofika kwenye klabu hiyo, lakini, alianza kujisikia vibaya tofauti na siku nyingine na kuongeza; "Yaani sikuwa na amani."

Alisema, "Mara, katikati ya maongezi tukaona mtu anaongea na simu. Ghafla tukiwa tunasema tuagane, wakaja watu kama watano hivi na bunduki, wakasema wewe na yule bwana mko free (huru), tunakuchukua wewe (Dk Ulimboka)," alieleza na kuongeza:

"Sijakaa sawa, nikaona nimeshaburutwa nikaanguka kwenye lami, wakaniinua na kuniingiza kwenye gari nyeusi, lakini halikuwa na namba."

Hata hivyo, jana Dk Ulimboka hakuonana na mwandishi wa habari hii, badala yake alirekodiwa, na Mwananchi kupata sauti yake akijibu swali kuhusu hali yake na tukio hilo, baada ya uongozi wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) kuzuia watu kumwona.

Daktari huyo wa magonjwa ya binadamu, amelazwa katika chumba cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU).

"Kidogo najisikia nafuu ikilinganishwa na nilivyokuja ingawaje, bado nina maumivu makali. Kwa hivyo, ingependeza niendelee na mapumziko na mtu yeyote anayetaka kuniona pengine hilo jambo lisifanyike sasa. Hivi sasa ni vizuri nipumzike," ilisikika sauti hiyo ya Dk Ulimboka.

Lakini, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa wodini alikolazwa Dk Ulimboka, kuna ulinzi mkali wa madaktari na hairuhusiwi watu kumwona kiholela siyo tu kwa sababu za kutaka aachwe apumzike, bali pia kutowaamini watu ovyo.

Madaktari wanaolinda eneo hilo walisikika jana wakisema, “Huyu tunamlinda wenyewe na haiwezekani mtu asiyefahamika kuingia humu ndani, na hilo tutahakikisha sisi wenyewe,”alisikika akisema mmoja wa madaktari hao.

Kiongozi jopo la madaktari

Katika hatua nyingine, kiongozi wa jopo la madaktari wanaomuhudumia Dk Ulimboka, Profesa Joseph Kahamba aliwaambia waandishi wa habari kuwa Dk Ulimboka ana majeraha mwili mzima.

“Ingawa kwa sasa anaendelea vizuri, Dk Ulimboka ameumia sana, kwani mwili wake mzima una majeraha kutokana na kupigwa na watekaji hao,”alisema Profesa Kahamba na kuongeza:

“Aliumia mbavuni,kifuani, miguuni, mikononi ambako aling’olewa baadhi ya kucha za vidole na kichwani na kinywani, ambako aling’olewa meno mawili,”alisema.

Alifafanua kwamba, kutokana na maumivu hayo ya kichwa, Dk Ulimboka alipata tatizo la mtikisiko wa ubongo, lakini akasisitiza kuwa madaktari bingwa wanaendelea na harakati za kuokoa maisha yake.

Uongozi wa Moi watoa neno

Uongozi wa Taasisi ya Mifupa (Moi) umeeleza kuwa hali yake inaendelea vizuri ingawa bado amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi cha taasisi hiyo.

Msemaji wa Moi, Almas Jumaa aliwaambia waandishi wa habari kuwa licha ya hali yake kuendelea vizuri, lakini haingewezekana kwa waandishi wa habari kuingia ndani ya chumba alikolazwa na kumwona Dk Ulimboka.

“Mgonjwa anaendelea vizuri ukilinganisha na jana (juzi), anaongea, anawatambua watu wanaokwenda kumwona, lakini utaratibu wa kwenda kumwona kwa ninyi imeshindikana kwa sababu yupo (ICU) ni chumba chenye utaratibu wake,”alisema Jumaa.

Jumaa aliongeza kwamba ili mtu aweze kuingia wodini analazimika kuvaa vazi maalumu na mavazi yaliyopo, yasingetosha, lakini pia wapo watu wanaoendelea kumpatia huduma ya matibabu.

Tamko la Jumuiya ya Madaktari

Wakati hali ya Dk Ulimboka ikiwa hivyo, madaktari wameipinga tume ya uchunguzi iliyoundwa na Jeshi la Polisi kuchunguza suala hilo, wakidai mazingira ya tukio hayaliondoi jeshi hilo kuhusika.

Katibu wa Jumuiya hiyo, Dk Edwin Chitage aliwaambia waandishi wa habari kuwa wangependa kuundwa kwa tume huru itakayofanya kazi ya kuchunguza tukio hilo na kutoa taarifa kwa umma.

“Madaktari kwa ujumla wetu tunalaani tukio la kutekwa nyara,kupigwa na kutupwa katika Msitu wa Pande, lakini pia hatuna imani na tume iliyoundwa na Jeshi la Polisi kwa sababu mazingira ya tukio hayaondoi kuhusika ama kutohusika kwa jeshi hilo,”alisema Dk Chitage.

Chitage alitoa msimamo wa madaktari kuwa ni kuendelea na mgomo, huku akionya Serikali kuacha vitendo vya kuwatisha, kwa madai kuwa vitendo hivyo haviwezi kuwa suluhu ya mgogoro kati ya pande hizo mbili.

“Kumekuwa na vitisho kwa madaktari katika maeneo mbalimbali nchini, hususan Dodoma, Mbeya, Arusha na Mwanza. Tunaionya Serikali kuacha mara moja na itambue kuwa mgogoro huo hauwezi kumalizwa kwa namna nyingine yoyote bali ni kwa Serikali kutekeleza madai ya madaktari,”alisema Chitega na kuongeza:

“Sisi madaktari kwa umoja wetu, tumechoka kushuhudia Watanzania wakipoteza maisha kwa magonjwa tunayoweza kuyatibu, kufanya kazi katika mazingira magumu huku kukiwa hakuna mipango ya kuboresha mazingira ya kazi, kukosekana kwa dawa na vifaa tiba.”

Mgomo huo wa madaktari leo unaingia siku ya saba tangu ulipotangazwa na mwenyekiti huyo kuwa, ungeanza rasmi Jumamosi iliyopita. 

Chanzo:   http://www.mwananchi.co.tz