Na Pamela Chilongola,Issa Lazaro (SJMC)
CHAMA Cha Walimu Tanzania (CWT), kimesema tukio la kutekwa nyara na baadaye kujeruhiwa kwa Dk Steven Ulimboka, linalenga katika kuwanyamazisha wanyonge wanaodai haki zao.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Rais wa chama hicho, Gratian Mukoba, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia Jumatano.
Katika tukio hilo watu wasiojulikana, walimteka nyara kiongozi huyo wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, akiwa katika viwanja vya Leaders Kinondoni na baadaye kupelekwa katika Msitu wa Pande ambako alipigwa na kujeruhiwa vibaya.
Tukio hilo limekuja wakati madaktari katika hospitali mbalimbali za Serikali, wakiwa katika mgomo usiokuwa na kikomo, wakishinikiza kulipwa maslahi bora.
Akizungumzia tukio hilo, Mukoba, alisema kitendo cha kutekwa nyara na kujeruhiwa kwa daktari huyo, si tu kwamba ni cha kuwanyamazisha wadai haki, lakini pia kimeidhalilisha Tanzania ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiheshimu katika kuheshimu haki za binadamu.
“CWT inalaani sana kitendo cha kumwagiza bure kwa damu ya Dk Ulimboka, Msitu wa Pande unatumika kutesa na kuulia watu wasiokuwa na hatia, msitu huo unapaswa kuwa kielelezo na alama ya Watanzania wanaoamka kupambana na dhuluma inayotekelezwa na idadi ndogo ya watu dhidi ya umma wa Watanzania,”alisema Mukoba
Mukoba alisema CWT inahamasisha misingi ya kutetea haki za jamii na wafanyakazi ambazo zimekuwa zikimomonyoka.
Wakati huo huo, baadhi ya wananchi katika Jiji la Dar es Salaam, wamesema tukio hilo lililenga katika kumyamazisha Dk Ulimboka, katika jitihada zake za kudai haki wa madaktari.
.
Wakizungumza kwa nyakati na mahali tofauti jana, wananchi hao walisema lengo la watu waliofanya unyama huyo ni kudhoofisha nguvu za Dk Ulimboka, ili asiendelee kudai haki.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi za Tiba cha Muhimbili (MUHAS), Furaha Alex, alisema kitendo hicho kimedhihirisha kuwa madaktari hapa nchini hawathaminiwi hapa wanapodai haki zao za msingi.
“Kitendo cha kupigwa kwa Dk Ulimboka, kimewadhalilisha sana madaktari hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa anawawakilisha wenzake. Hili ni jambo la kusikitisha saba,” alisema Alex. ( CHANZO: MWANANCHI)