Friday, June 29, 2012

TAMKO FUPI LA JUMUIYA YA MADAKTARI KWA WAANDISHI WA HABARI

KAMATI YA JUMUIYA YA MADAKTARI TANZANIA
                                                                                                                                                                                                                
YAH: TAMKO FUPI LA JUMUIYA YA MADAKTARI KWA WAANDISHI WA HABARI LEO TAREHE 28.06.2012 
Madaktari wote hatuna imani na tume iliyoundwa na Jeshi la polisi nchini yenye lengo la kuendesha uchunguzi juu ya kutekwa, kunyanyaswa na kupigwa vibaya kwa Dr. Ulimboka Stephen na tunataka chombo huru kiundwe ili kupata ukweli wa tukio hilo.
Pia tunakemea na kuonya juu ya vitisho vyote vinavyotolewa na baadhi ya watawala katika taasisi mbalimbali dhidi ya madaktari mfano Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Bugando, Mbeya na kwingineko ambapo wametishwa na kufukuzwa kwa kutumia mabavu.
Madaktari tunazidi kusisitiza kuwa hakuna njia nyingine yeyote ya kusuluhisha mgogoro huu isipokuwa ni kwa kutekeleza madai na hoja za msingi za madaktari kwa njia ya mazungumzo ya dhati.
Madaktari tumechoka kuona huduma za afya nchini zikizidi kudorora mwaka hadi mwaka, Tumechoka kuona wagonjwa wakilala chini na watoto wakilala wanne katika kitanda kimoja Tumechoka kuona msongamano mkubwa kwa wagonjwa katika hospitali zetu huku kukiwa hakuna mpango wowote wa uboreshaji.
Tumechoka kuona wagonjwa wakikosa dawa, vipimo sahihi na watumishi wa afya wakifanya kazi katika mazingira magumu yanayoviza ubora wa huduma na misingi ya taaluma. Kwa hiyo, kwa moyo wetu leo tumejitolea kutetea uboreshaji wa sekta ya afya licha ya vitisho tunavyoendelea kuvipata.
Rai kwa Madaktari; Madaktari wote kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu, tunashukuru madaktari wote kwa ushirikiano na kuendelea na mshikamano.
Imetolewa na Kamati ya Jumuiya ya Madaktari.