Thursday, June 21, 2012

Bajeti mbovu jinsi itakavyochangia mfumuko wa bei

Joseph Zablon
KATIKA Bajeti ya Serikali ya mwaka ujao wa  2012/2013, Serikalli imetenga Sh128.4 bilioni kwa ajili ya kuimarisha viwanda vidogo nchini na sekta hiyo ambayo siku za nyuma ilitoa kiasi kikubwa cha ajira hususan kwa vijana.
Waziri wa Fedha na Uchumi Dk William Mgimwa anasema bajeti ya sasa imelenga kutanzua kero mbalimbali katika sekta ya viwanda. Pia bajeti hiyo imekusudia kuendeleza viwanda ambavyo vinatumia malighafi za ndani na vinavyoongeza thamani ya madini.
Viwanda vingine anavitaja kuwa ni pamoja na viwanda vikubwa vya saruji na vile vya teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Hatua ya kuboresha viwanda hivyo itaenda sanjari na viwanda vidogo ambavyo vimetengewa kiasi hicho cha fedha.
Mkurugenzi wa Sera na Ushawishi wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Hussein Kamote anasema bajeti hiyo pamoja na mambo mengine, imeendelea na desturi ya kutegemea wahisani katika kutekeleza miradi mingi kwa mfano, miundombinu na nishati.
Anasema nishati na miundombinu ni roho za viwanda vya uzalishaji nchini, lakini imekuwa ni kawaida kutegemea wahisani kuendeleza miradi wakati wakati fedha za matumizi ya kawaida, zikitoka katika vyanzo vya uhakika vya ndani.

"Ili kunusuru viwanda kuna haja ya kutenga mafungu ya kutosha kwa ajili ya sekta za reli, bandari na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), taasisi ambazo ni kiungo muhimu cha uchumi wa wananchi wa kawaida na wenye viwanda pia," anasema.

Kamote anabainisha kuwa hivi sasa wenye viwanda na wadau wengine wa masuala ya uchumi wanalazimika kutumia gharama kubwa ya usafiri wa magari kusafirisha mizigo kutoka eneo moja hadi lingine wakati njia yenye gharama nafuu ambayo ni treni, haitumiki.

Anasema usafiri wa reli ni rahisi na wa gharama nafuu kwamba reli imekuwa ikisafirisha shehena kubwa zadi kuliko magari. Anasema usafiri wa reli utaleta maendeleo ya kiuchumi haraka.

Kamote anasema bajeti ya kutosha katika reli, barabara, bandari na miundomninu miggine itasaidia kuzuia mfumuko wa bei nchini kwa kuwa bidhaa zitawafikia walaji kwa bei nafuu tofauti na sasa.
Mkurugenzi huyo anasema kuachwa kwa kodi katika maji na kodi zilizopo katika mafuta ikiwamo petroli na dizeli hakujatoa ahueni kwa wananchi.
Dk. Prosper Ngowi ambaye ni mchambuzi wa masuala ya uchumi anasema kutokuwapo kwa umeme wa uhakika, maji na miundombinu isiyoeleweka kumechangia mfumuko wa bei.
Anasema mwaka jana mfumuko ulifika asilimia 19.4 ikiwa ni wastani maradufu wa asilimia nne ambazo zinakubalika kiuchumi.

Lakini lengo la bajeti iliyotangazwa bungeni wiki iliyopita ni kupunguza mfumuko huo hadi asilimia 18.4 .
"Walitumia mbinu ya kuongeza fedha katika mzunguko ili kudhibiti mfumuko wa bei, dhana ambayo siyo sahihi kwani sababu za mfumuko zipo wazi ambazo ni matatizo ya upatikanaji wa nishati ya umeme, miundombinu ya barabara na kutegemea mvua katika kilimo," anasema.
Mchambuzi huyo anasema kauli ya waziri wa fedha kwamba tutakopesheka na kubainisha kwamba deni la Taifa linaweza kubebeka kunamezwa na kasi ya ukuaji wa deni hilo.

“Serikali kutegemea kwamba itakopeshwa ili iweze kutekeleza mipango yake ya maendeleo ni makosa,” anasema.
Anaeleza jaribio ambalo Serikali inataka kulifanya hivi sasa lilijaribiwa mwaka 2009 na kuomba mkopo wa dola 500 milioni za Marekani katika soko la dunia, lakini uchumi haukuruhusu hivyo hawakupewa.
"Inachotaka kufanya ni lazima kuwaleta wataalamu wa masuala ya uchumi ambao watakuja kutuhakiki ikiwa ni pamoja na kuangalia kama tunakopesheka, pato la taifa na ukuaji wa deni la nje ukoje" anasema.
Kama kutakuwa na walakini, hasa kama deni linakua kwa kasi maana yake ni kwamba tutakopeshwa kidogo na ikibidi riba itaongezwa, lakini kabla ya kufika huko tunapaswa kuangalia ukuaji wa deni unaendeleaje.

Anasema deni hilo linatishia ustawi wa viwanda nchini na Serikali kuendelea kuwa maskini kutokana na kushindwa kukusanya kodi ipasavyo.  Utafiti wa hivi karibuni unabainisha kuwa suala la mapato ni tatizo la kimsingi.
Dk Ngowi anasema katika utafiti wake ambao upo katika kitabu ambacho amekizindua hivi karibuni na viongozi wa dini ya kikristu, kiitwacho ‘One Bilion Dollar Question’, amebainisha kwamba Serikali imepoteza dola 1 bilioni za Marekani kila mwaka kutokana na watu wengi kutolipa kodi.

"Watu ambao wanastahili kulipa kodi nchini ni milioni 15, lakini wanaolipa ni milioni 1.5, hiyo ina maana kuwa wengine milioni 13.5 hawalipi kodi," anasema.

Anabainisha kwamba kodi zote kayika bajeti hiyo ni sawa na asilimia 21, lakini kodi inayokusanywa ni asilimia 16 tu.
Anasema mikakati ya sasa ni kukusanya  asilimia 18 na kwamba asilimia tano hadi sita haikusanywi katika asilimia 21.

Dk Ngowi anasema sekta binafsi inachukua kati ya asilimia 60 mpaka 70 ya uzalishaji nchini, lakini kundi hilo halilipi kodi za Serikali na kudhohofisha viwanda vya uzalishaji.

Anasema utafiti wa Benki ya Dunia (WB) unabainisha kwamba Tanzania ni nchi ya mwisho Afrika Mashariki kwa kutoa taarifa kidogo za mauzo. Pia asilimia 69 pekee ya wafanyabiashara ndio wanawasilisha taarifa zao wakati wengine asilimia 31 taarifa zao hazijulikani.
Ripoti hiyo ya benki ya dunia inaitaja Kenya kuwa ni nchi ambayo wafanyabiashara wake wanaongoza kwa kuwasilisha taarifa za mauzo yao kunakohusika kwa asilimia 88 na kufuatiwa na Uganda kwa asilimia 77.
Sekta isiyo rasmi wanaotoa taarifa ya mauzo yao kwa asilimia 19 tu kwa mfano, iwapo mjasiriamali ameuza bidhaa na kupata Sh100 basi anatoa taarifa za Sh19 tu na kiasi kinachobaki kinakwenda kusikojulikana.
Mwenyekiti wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye anasema uwiano hauleti matumaini kwamba siku za usoni kutakuwa na mazingira bora ya biashara hususan suala la miundombinu.
Anasema katika bajeti ya mwaka jana 2011 zilitengwa Sh2.7 trilioni, lakini mwaka huu Sh1.5 bilioni kwa ajili ya kuanzisha reli, bandari na barabara mbali na umeme.

Simbeye anasema fedha zilizotengwa sasa ni pungufu ukilinganisha na bajeti iliyopita kwa silimia 49 na haieleweki kama wamefanya hivyo kwa kuwa tumeendelea kidogo.

"Waziri Mgimwa katika kitabu chake cha bajeti anakiri kwamba mwaka jana hawakuweza kufikia lengo kutokana na kukosa fedha za wahisani hivyo ni wazi kwamba kutegemea wahisani hatuwezi kuchuja kiwango cha maendeleo yetu," anasema.

Kutokana na hali hiyo Serikali ina wajibu wa kuwasikiliza wadau wa masuala ya kiuchumi na ikibidi kufanyia marekebisho bajeti iliyotangazwa.

“Wakati mwingine ni vizuri kuwashirikisha wadau hao na michango yao kufanyiwa kazi ili kupata bajeti nzuri ambayo itakua na dira ya kueleweka.

Tofauti na hivyo huenda mfumuko wa bei utazidi kupanda na siyo ajabu ikafanya riba nazo kuongezeka katika taasisi za fedha na kuchangia ukuaji wa deni la taifa hali ambayo itafanya maisha ya mtanzania wa kawaida kuwa magumu kuliko ilivyo sasa.