Kufuatia mahojiano kati ya kipindi cha Amplifaya cha Clouds Fm na Hamis Mwinjuma aka MwanaFA, Mwenyekiti mtendaji wa B’Hits Music Group Ltd, amemuandika barua mtangazaji wa kipindi hicho Milard Ayo kutoa ufafanuzi juu ya kilichoongewa na MwanaFA. Habari hiyo pia iliandikwa kwenye blog ya Milard tarehe 10, June, 2012. Wakati wa kutuma barua hiyo, Hermy B ametutumia pia na hivi ndivyo anavyosema:
Ningependa kutoa ufafanuzi wa habari iliyoandikwa na blog
yako kufuatia mahojiano yako na mwana F.A. Nirejee kwamba mahojiano hayo
yanasema kwamba Studio ya kurekodi muziki ya Kampuni ya Bhits imepandisha bei
ya kurekodi, na bei hiyo ndiyo chanzo cha AY na F.A kuhamishia kazi zao sehemu
nyingine.
Baada ya kusoma makala hiyo inayonihusu mimi binafsi na
kampuni ya Bhits kwenye blog yako nimeona umuhimu wa kujibu makala yako kwani
kwa mtu mwingine anaweza kuona ni kitu cha kawaida lakini kwangu naumia kwa
sababu maneno hayo yameshaweka na yanaendelea kutia hofu wateja wangu hasa hawa
wa muziki kwa kuwafanya wajihisi hawana hicho kiwango cha fedha, kurekodi
muziki pale Bhits.
Kitu ambachao hakifahamiki ni kwamba hata Mwana FA kama
ilivyo kwa A.y nae alinitafuta kwa njia ya simu mwanzoni mwa mwaka huu
akinitaka nimuuzie nyimbo zake alizorekodi kwangu kwa utaratibu wa reja reja
kama vile alivyohitaji A.Y, lengo likiwa ni kuzindua albamu hiyo na kuiuza. Bei
aliyotaka kulipa ilikua pia ni ile ile ya kujilinganisha na msanii mdogo
anaehangaika kutoka.
Kitu kingine kilichofanya tushindwane kibiashara ni pale F.A
alipodai bei hiyo ndogo itahusika katika kumuuzia pia haki zote za muziki huo,
yani za kwake na zangu. Kwa namna nyingine niliombwa nikane haki zangu za
muziki kama Producer na muziki huo uwe mali ya Mwana FA moja kwa moja, akiwa na
haki ya kuuza, kuukodisha na kufanyia biashara yoyote ile anavojiskia yeye bila
mimi kuhusika.
Na mimi nikitaka kutumia hata mdundo wa wimbo huo nitahitaji
kumuomba ruhusa yeye labda hata kwa malipo na kinyume cha hapo ana haki ya
kunipeleka mahakamani kunishtaki kwa wizi.
Nilishangazwa kwa kitendo cha FA kudhani kuwa naweza kukana
haki zangu za kimuziki kwa sababu ya tamaa ya pesa ndogo, nasema kwamba ni hela
ndogo ukilinganisha na thamani ya haki zangu za muziki ambazo huko mbele siwezi
jua zitanisaidia vipi. Mabishano haya ya bei yaliendelea mpaka tukafika sehemu
nikamwambia Mwana F.A anipe Milioni Moja kwa wimbo mmoja ataochukua kwangu kwa
ajili ya albamu yake. Akanambia tuma mkataba lakini aliongeza maneno “bei yako
sio ya kihalisia”. Mkataba huo ulikuwa na kifungu cha kudumisha urafiki wetu
ambacho kinaeleza kuwa, “mauzo ya albamu ni mali ya msanii, akiamua kunipatia
chochote hewala lakini mkataba huu haumlazimu”, lakini hakusaini mkataba huo.
Nachojiuliza neno kupandishiwa bei lina maana gani? Kwani si
lazima uwe na bei ya mwanzoni ili inayofata iwe kubwa zaidi? Sasa kama wasanii
hawa kwangu walikua wanarekodi bure na hawalipi hata senti ya umeme wala
software ambazo mimi nimekua nazilipia hela nyingi kwa mwezi kuzifanya zipate
leseni ya kufanya kazi watakua vipi na haki ya kusema wamepandishiwa bei?
Katika barua iliyopita nimesema kwamba fedha niliyopata
kutokana na muziki wao haizidi milioni tatu kwa miaka yote minne niliyokuwepo
nao.
Siifahamu na sijawahi kuwatajia hiyo bei ambayo inaweza
kuwafanya A.Y na F.A warekodi nyimbo za kutosha hata nje ya Tanzania.
Bei ya
Bhits wateja wake wanaifahamu na ipo pale pale kwa kila mtanzania kumudu. Ubora
wa muziki wetu wasanii wanaujua pia na kwa anayependa kurekodi kwetu
anakaribishwa kwa kuwa hatubagui na ambaye hajaridhika na viwango vyetu vya
ubora na bei, hili ni soko huria anaweza kuchagua sehemu nyingine kwa amani
kabisa.
Watu wanaweza wakaona mimi ni mchochezi na mgomvi lakini
itambulike hili swala lilikwisha tokea February mwaka huu nikiwa mimi ndiye
niliyeumizwa na nikaamua kukaa kimya. Nashindwa kuelewa kwa nini wao wameamua
kuongelea makubaliano yetu binfasi kwa media tena kwa kuyageuza maneno.
Itambulike kuwa mara ya kwanza kabisa hili linasikika kwa
media niliwatafuta kwa simu ndugu zangu hawa nikawaambia kuwa hakuna haja ya
Kuongea kwa kuwa yameshakwisha tukae kimya tulindane.
Lakini naona wanaendelea
kuongea uongo huo ambao unaniumiza mimi na kampuni ya B Hits kibiashara.
Biashara zipo nyingi bado na labda huko mbele tutakutana
tena, hakuna haja ya kuharibu kila kitu leo
kwa vitu vidogo kama hivi halafu kesho pia tupoteze nafasi ya kufanya
mambo makubwa, ombi langu ni kwamba tuachane kwa amani. Haswa ukitegemea hatuna
mkataba wa maandishi kati ya mimi, Mwana F.A na A.y nafikiri kuachana ni kitu
rahisi na cha amani na kisichohitaji nguvu wala maumivu kukitimiza.
Namalizia kwa kusisitiza kuwa niliyoyasema ni ya ukweli na
itakaponilazimu kutoa ushahidi nitafanya hivyo.
Wasalaam
Hermes Bariki Joachim (Hermy B)
Managing Director