Monday, June 25, 2012

SAID FELLA NA BAB TALE NDO INJINI YA MAFANIKIO YA DIAMONDKATIKA utata ulifunikwa kwa muda mrefu kuhusiana na meneja au msimamizi wa kazi za msanii mwenye mafanikio nchini Tanzania, Nassib Abdul a.k.a Diamond  umeibua hoja baada ya kampuni ya Osata kuibuka na kudai kuwa wao ndio wasimamizi wa baadhi ya kazi za msanii huyo.

Kampuni hiyo inayomilikiwa na Saidi Fella na Babu Tale, imeelezwa kuwa inajihusisha na usambazaji pamoja na matangazo ya kazi za wasanii katika vituo vya habari jijini Dar es Salaam na katika vituo vilivyopo Mikoani ambako huwawia vigumu wasanii kuvifikia.

"Naweza kusema tunajitahidi katika suala la matangazo kwa kweli ingawa Diamond mwenyewe anajisimamia katika mambo mengi, lakini tunachukua nafasi kubwa kuhakikisha anayafikia malengo ambayo hata yeye mwenyewe anajituma kuyafikia" anaanza kwa kusema Babu Tale ambaye pia ni meneja wa Tip Top Connection.

Katika suala la usambazaji, Tale anasema hawana ruhusa za kusambaza albamu za msanii, bali wao wanasambaza kazi ya msanii katika vituo vya redio na televisheni, pamoja na kuwatangaza katika vyombo vya habari.

"Kuna utofauti mkubwa sana katika suala la matangazo na usambazaji kati yetu na msambazaji wa albamu, sisi tunamtangaza msanii na kusambaza kazi zake, unajua hivi sasa kuna zaidi ya vituo 80 vya redio hapa nchini, hii si rahisi msanii kuvifikia, lakini sisi tunavifikia na hata video pia tunaisambaza kwa zaidi ya televisheni 25 zilizopo hapa nchini" anasema.

Hata hivyo Tale anabainisha wazi kuwa katika ufanisi wa kazi zao mara nyingi hawana mkataba na mhusika "mfano Diamond hatuna mkataba naye, lakini tuna makubaliano yetu ambayo tunayafanya tukiwa naye, na linapokuja suala la malipo ni kati yetu wawili" anasema bila kutaja kiwango cha malipo wanayokubaliana.

“Hata katika ziara ya Big Brother, OSATA tulipigiwa simu na Big Brother wakitutaka tumpeleke msanii anayefanya vizuri na ndipo tukamchagua Diamond, tulifanya makubaliano na kwa uzuri tulichagua mtu sahihi kampuni inajivunia kwa hilo” anasema.

Naye Saidi Fella anasema kuwa kampuni yao imejitanua mpaka nje ya nchi ukilinganisha na hapo awali "Tulianza mwaka 2010 kwa kusambaza kazi za wasanii lakini hivi sasa tumejitanua zaidi Afrika Mashariki na bara zima la Afrika na hivyo ikitokea msanii anapeleka kazi zake basi kuna malipo pia inategemeana na wapi.

Anasema na kuongeza "msanii hawezi kufanya kila kitu, anahitaji msaada kutoka kwa wasimamizi mbalimbali na hiyo ndiyo siri ya mafanikio kwa wasanii wengi ambao mpaka sasa bado wapo katika gemu, huwa hakuna maisha kwa msanii ambaye hana usimamizi wala washauri mara nyingi” anasema Fella.