Tuesday, July 31, 2012
Benki ya CBA kuisaidia Zanzibar kununua Meli mpya
Na Mohammed Mhina, Zanzibar Wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa kwenye mchakato wa kutafuta fedha za kununua meli mpya, Benki ya Biashara ya Afrika (CBA), imesema iko tayari kuikopesha SMZ fedha za kununulia Meli hiyo.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo Bw. Yohane Kaduma, amesema benki yake iko tayari kuipitia SMZ mkopo wa kununulia Meli hiyo endapo watakubaliana na kushirikishwa kwenye mchakato huo.
Bw. Kaduma alikuwa akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Zannzibar mara baada ya kukabidhi msaada wa shilingi milioni 5, kwa Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibat Balozi Seif Ali Iddi ili kusaiidia ghala za matibabu kwa majeruhi na ubani kwa wafiwa wa ajali ya Meli ya Skagit.
Bw. Kaduma amesema kuwa endapo Benk yake itaombwa kutoa mkopo huo inaweza kufanya hivyo ili mradi tu kukaa meza moja na Serikali na kukubaliana aina ya mkopo pamoja na mambo mengine.
Awali akipokea msaada huo, Makam wa pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, amesema kuwa pamoja na kusimamishwa kwa baadhi ya meli za watu binafsi kuchukua abiria, SMZ pia imeagiza meli zake kufanyiwa uchunguzi kama zinafaa kuchukua abiria.
Balozi Seif amesema kuwa ameziagiza Mamlaka ya usafiri majini Zanzibar na Sumatra, kuzifanyia uchunguzi meli hizo za SMZ ikiwemo MV Maendeleo ambayo imerejea siku za karibuni ikitokea Mombasa nchini Kenya ambako ilikuwa katika matengenezo makubwa.
Amesema Serikali haiwezi kukaa kimya huku ikiona kuwa wananchi wake wanapatwa na majanga ya mara kwa mara kutokana na kusafiri kwa meli zisizo na uhakika.
Katika hatua nyingine idadi ya maiti za MV Skagit, imeongezaka hadi kufikia 128 baada ya maiti nyinine mbili kupatikana leo karibu na Kisiwa cha Chumbe nje kidogo ya mji wa Zanzibar na nyingine sita zikipatikana mkoani Tanga.
Tofauti na taarifa za awali kuwa maiti tano zilipatikana Bagamoyo mkoani Pwani, ifahamike kuwa maiti hizo zilipatikana katika fukwe za bahari wilayani Pangani na nyingine mjini Tanga.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Kamanda wa Polisi mkoani Tanga ACP Costantine Masawe, maiti nne ikiwemo ya mwanamke mmoja zilipatikana huko Pangani na nyingine mbili ikiwemo ya mwanamke mmoja zikapatikana kwenye fukwe za bahari mjini Tanga.
Kamanda Masawe amesema kuwa maiti zote zilichukuliwa vipimo kwa ajili ya uchunguzi wa Vinasaba (DNA) pamoja na kupigwa picha kabla ya kuzikwa.
Hata hivyo Kamanda huyo wa Polisi amesema kuwa maiti moja kati ya hizo, ilitambuliwa kuwa ni ya Mohammed Saidi Salum mkazi wa Ziwani Chakechake mkoa wa Kusini Pemba ambaye alitambuliwa baada ya simu aliyopatikana nayo kufanyiwa uchunguzi.
Hadi sasa maiti ambazo hazijapatikana ni 16 kutokana na kupatikana kwa watu 146 wakiwa hai ikilinganishwa na idadi ya watu 290 waliokuwemo ndani ya meli hiyo ya Skagit siku ya tukio.