Sunday, July 1, 2012

Habari njema kwa wagonjwa wa ukimwi

BBC, London
WAGONJWA  wa Ukimwi  huenda wakanufaika na dawa mpya ambayo itawawezesha kutumia tembe moja kwa siku. Hii ni kwa mujibu wa utafiti mpya nchini Marekani.

Kwa mujibu wa Jarida la Afya Lancet lililonukuliwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), limesema tembe hiyo mpya imetengenezwa kwa kutumia aina nne ya Dawa za Kupunguza Makali ya Virusi vya Ukimwi (ARV).

Kulingana  na utafiti huo, dawa hiyo mpya itawarahisishia wagonjwa katika kuhakikisha wanafuata maagizo ya madaktari wao.

Ukimwi hauna tiba lakini watafiti wameweza kutoa dawa za kukabiliana na maradhi yanayomnyemelea mwathirika kutokana na kushuka kwa kinga yake ya mwili.

Mtafiti Mkuu katika Hospitali ya Wanawake ya Brigham huko Boston, Massachusetts,  Paul Sax, ambaye pia ni mwanazuo wa ziada wa taasisi ya afya ya Harvard, ameelezea umuhimu wa tembe hii kuwa itaimarisha afya ya wagonjwa.

Dk Sax ameongoza utafiti huu ambapo pia wamefanyia majaribio tembe hii kwa wagonjwa 700 na kusema inafanya kazi, japo kulitokea matatizo ya figo miongoni mwa waliotumia.

Licha ya mafanikio ya sasa watafiti wanasema raia wengi hawafahamu hali zao ambapo wameendelea kuishi na maambukizi bila kujua.