Monday, July 30, 2012

MUDA WA VITAMBULISHO VYA TAIFA WAONGEZWA


Benjamin Masese na Christina Gauluhanga, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeongeza muda wa wiki moja kwa wakazi wa Dar es Salaam wenye sifa ya kupatiwa vitambulisho hivyo.

Taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana na Mkurugenzi wa NIDA, Dickson Maimu alisema shughuli hiyo itamalizika Agosti 6, 2012 huku akisisitiza muda mwingine hautaongezwa tena.

Maimu alisema wageni wote wanapaswa kujaza fomu 2A kwa kueleza ukweli uraia wa nchi zao na hadhi ya ukaazi wao.

Alisema kwa mujibu wa sheria za usajili na utambuzi wa watu kifungu cha 9 (2) waombaji wasiojua kusoma na kuandika watasaidiwa kujaziwa fomu na wale wanaojua kusoma na kuandika watapewa fomu ili kujaza wenyewe chini ya usimamizi wa usajili wa kituo husika.

Maimu alisema kwa mujibu wa kifungu cha 20 (1) C inaeleza kwamba ni kosa la jinai kutoa taarifa ambazo si sahihi zikiwamo za uraia na kuongeza atakayebainika atatozwa faini au kwenda jela miaka isiyozidi mitatu.

Vile vile alisema watu walio katika makundi maalumu kama wazee, walemavu na wagonjwa watapelekewa mahitaji yao pale walipo na viongozi wa Serikali za mitaa.

AWALI kabla ya kuongezwa kwa muda huo shughuli hiyo ilikuwa imeonekana kukwama kutokana na kujitokeza kasoro kadhaa zilizosababisha baadhi ya wananchi kushindwa kujiandikisha.

Wakizungumza jana na MTANZANIA kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi waliojitokeza kujiandikisha katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam, wamesema NIDA haikuweka utaratibu mzuri jambo ambalo linaonekana kusababisha wananchi kukosa haki ya kujiandikisha kwa siku zilizopangwa.

Mkazi mmoja wa Mongola la Ndege, Herbert Masamu amesema shughuli hiyo imekuwa ngumu kutokana na uchache wa watu waliopangwa kuandikisha taarifa za wananchi jambo ambalo limesababisha msongamano katika vituo mbalimbali.

Alisema pia kukosekana kwa elimu ya kutosha za nyaraka au taarifa muhumi anazotakiwa kuwa nazo mwananchi anayekwenda kujiandikisha nalo limekuwa ni kero kwa wananchi hivyo kulazimika kwenda na kurudi katika vituo vya kuandikisha bila kufanikiwa kujiandikisha.

“ Katika hili la uchache wa watu wanaoandikisha limetusababishia usumbufu hivyo NIDA wanapaswa kuongeza siku na idadi ya waandikishaji kama ilivyo kwenye kitambulisho cha kupigia kura ili kila mwananchi apate haki ya kujiandikisha,”alisema Masamu.

Kiwalani

Katika siku mbili za Jumamosi na Jumapili,MTANZANIA ilifanikiwa kufika katika vituo mbalimbali kikiwamo cha Hali ya Hewa kilichopo kata ya Kiwalani na kushuhudia umati wa watu wengi wakisubiri huduma hiyo bila mafanikio.

Katika kituo ambacho hicho kinachounganisha zaidi ya mitaa mitatu, kulikuwa na hali ya kushangaza kutokana na wananchi kufika kituoni kuanzia saa 12 alfajiri ili kuwahi kujipanga foleni huku wafanyakazi wa NIDA hawaoneki kituoni.

Katika kituo hicho, mwandishi wa gazeti hili alikuwa ni mmojwapo ya wanaohitaji kuandikishwa lakini hakuweza kupata fursa kutokana na waandikishaji kuchelewa kufika kituoni na kufanya kazi pole pole.

Hata hivyo ilipofika saa 3.13 asubuhi alionekana Mwenyekiti wa Mtaa wa Minazi Mirefu, Ubaya Chuma na kuanza kutoa maelekezo kwa wananchi utaratibu uliopo .

Licha ya kutolewa maelekezo hayo lakini wafanyakazi hao hawakutokea hadi ilipofika saa 3 .27 asubuhi ndipo wandikishaji watatu walionekana hapo na kuanza huduma huku mtu mmoja akichukua kati ya dakika 20 na 30 kuandikishwa.

Katika kituo hicho cha Hali ya Hewa ilielezwa kwamba kuna waandikishaji 10 lakini hadi inafika saa 10 .03 walikuwa wamefika saba kitendo ambacho kilisababisha ongezekao kubwa la wananchi huku wakilalamika. 

Wakizungumza na MTANZANIA baadhi ya wananchi walisema msongamano huo unasabishwa na wafanyakazi wa NIDA kuchelewa kufika kituoni pamoja na utaratibu uliowekwa. 

Wananchi hao walililamikia kituo kutokana na na kuwapo na matatizo mengi yakiwamo kitabu kuibiwa cha orodha ya wananchi kitendo kilichomlazimu Chuma kuweka utaratibu wa kuwatambua wananchi hao.

Vile vile katika kituo hicho kuina wananchi walipatikana wakiwa na photocopy ya kitambulisho cha kupigia kura cha mtu mwingine wakitaka kukitumia.

Kwa mujibu wa Ubaya aliwaeleza wananchi hao kwamba kuna watu wachache wasio wadilifu wanachukua kadi za kupigia kura za watu wengine na kubandua picha za mtu halali na kubandika za kwao kisha kuzitoa photocopy.

Chanzo: Mtanzania