Hivi
majuzi niliskia kuwepo kwa tuzo za waandishi wa habari za mtandaoni
maarufu kama waandishi wa magazeti tando (blogs). Katika Tuzo hizo
ambazo ziliandaliwa kwa vigezo wanavyovijua Vodacom, wametajwa washindi
fulani. Kama mdau wa kawaida katika magazeti tando, miongoni mwa waasisi
wa Bloger wa kwanza kabisa wa Kitanzania naamini kwa sasa kama nchi hii
itakuwa inaendeshwa kishkaji, kirafiki, kima kundi na ikaachwa bila
kukemewa basi siku si nyingi tutapoteza ladha ya mashindano yanayopima
viwango na ubora wa kazi hali itakayofanya nchi kubakia kuwa ya
wababaishaji kila siku.
Eneo hili la magazeti tando niliwahi kulilalamikia kutokana na
kukosekana ubunifu hasa inapotokea habari moja inajaa kila blog kama
ambavyo ipo katika magazeti ya Tanzania. Kwa kuona hili hili nashangaa
blog iliyo na kazi ya kubandika picha za magazeti ya kila siku ama
habari za wasanii walio nje au kuchota mawazo ya watu katika FB na
twitter, au kusubiri taarifa za Maafisa Habari ikaibuka mshindi kwa kuwa
tu eti inaonesha kuwa na wasomaji wengi. Kwamba hamjui kuwa ukiseti
weblog yako ihesabu wanaoitembelea itahesabu bila kujali ni nani
anaingia mara ngapi?
Kwa mantiki hii kigezo cha idadi ya watu si muwli kuonesha kuwa huyu ni mahiri katika kutoa taarifa katika Blog yake.
Natoa rai, kuwa mliopata nafasi ya kuwa na nguvu katika makampuni
msitumie nafasi hizo vibaya kwa kutaka kuidhinisha udhamini wa blog kwa
rafiki zenu na kisha kupoteza ladha ya ubunifu katika blog. Najua
mmefanya hivi sana katika maeneo kama ya sanaa za urembo na kwingineko
lakini kumbukeni hili limezidi na haliwezi kuvumiliwa! Jamhuri hii
ilikuwepo kabla yenu na hiki mnachojivunia kwa kuwa kimetengenezwa na
urithi wa Baba zenu msitarajie kitabaki kuwa hivi kila siku. Tendeni
haki japo kidogo jamii hii itawaheshimu.
Kwa masikitiko na hasira kidogo nawasilisha!
Bonny Makene Road to PhD.