Wednesday, August 1, 2012

Wasanii wapiga marufuku matumizi ya ringtone zao, wayapa makampuni ya simu siku saba
Umoja wa wanamuziki wa Bongo Flava, Rhumba, Dance, muziki wa Injili na aina zingine leo umetoa agizo kwa makampuni yanayouza miito ya simu nchini pamoja na makampuni ya simu kuiondoa miitio hiyo ndani ya siku saba kuanzia leo mpaka pale watakapokubaliana mikataba mipya.

Katika barua hiyo iliyoandikwa kwenda kwa waandishi wa habari na iliyosainiwa na wasanii zaidi ya 150 nchini, wasanii hao wameyataka makampuni ya simu kuondoa matangazo ya ringtone hizo kwenye radio, magazeti, tv, website na kwenye ujumbe mfupi wa simu.

Hatua hiyo imechukuliwa na wasanii hao baada ya kubaini kuwa makampuni ya simu yanawanyonya kwa kiasi kikubwa kwa kuwalipa chini ya asilimia 10 ya mauzo ya ringtone hizo huku yenyewe yakibaki na zaidi ya asilimia 80.

Wiki iliyopita mbunge wa Kigoma Zitto Kabwe aliliibua suala hilo bungeni na kudai kuwa imeundwa kamati itakayoangalia upya utaratibu wa mauzo ya ringtone.

Press Release ndio hii.

YAH: KUFUTA MIKATABA NA KUSIMAMISHA KUUZA MUZIKI WA BONGO FLEVA,GOSPEL,DANSI NA TAARABU KWENYE MITANDAO YA SIMU.
Husika na kichwa cha habari hapo juu,
Kwa ujumla wetu sisi Wasanii toka Tanzania tunaofanya muziki wa Gospel, Rhumba , Taarabu pamoja na Bongo fleva tumeamua kutoa agzio kwenu la kusimamisha mauzo ya kazi zetu za muziki katika mtindo wa Ringtone na Callertunes katika mitandao ya simu ya Vodacom, Zantel,Tigo na Airtel na kufuta mkataba tuliosaini kati yetu sisi Wasanii na Kampuni yako mpaka hapo tutakapokaa sisi kama wasanii, nyinyi kama wasambazaji wa muziki wetu, pamoja na Mitandao ya simu ili kuzungumzia namna mpya ya sisi na nyinyi tutakavyofanya kazi.
Sababu ya sisi Wasanii kusimamisha na kufuta mikataba kati yetu na wanaofanya biashara ya kuuza maudhui yetu ni pamoja kampuni husika kushindwa kuweka wazi taarifa za mauzo ya nyimbo pamoja na kutolipa katika muda husika kama ilivyoanishwa katika mikataba husika.
Sababu ya pili ni mitandao ya simu kuchukua kiasi kikubwa cha fedha ambacho ni asilimia themanini ya mauzo yote ya maudhui yetu, jambo hili linatuumiza na limetufanya tuendelee kuishi kwa kutegemea aina moja ya pato toka kwenye shoo.
Hivyo tumeziagiza kampuni zote zinazofanya kazi ya kuuza maudhui yetu kutoa maelekezo kwenye mtandao husika kuwaelekeza kusimamisha mauzo ya kazi zetu za sanaa ndani ya siku saba kuanzia leo tarehe 30/07/12 ikiwa pamoja na kusimamisha matangazo yote yanayotangaza mauzo ya kazi zetu kwa njia ya Television , Radio , blogs, website, Magazeti na Ujumbe Mfupi wa maneno mpaka hapo tutakapofikia muafaka.
Jumla ya wasanii 153 wameshasaini barua hizo na wengine wanaendelea kusaini.
Mwisho tunawashukuru kwa ushirikianao wenu, na tunaambatanisha sahihi zetu ili kuonyesha uthibitisho wa umoja wetu katika jambo hili.
Asante.