Mwandaaji wa Shindano la Bongo Star Search (BSS) Ritha Paulsen akisisitiza jambo wakati wa kikao cha tathimini cha shindano hilo kilichofanyika mwishoni mwa wiki hii makao makuu ya BASATA. Kulia ni Mratibu wa shindano hilo kutoka BASATA, Vick Temu.
Makamu wa Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania Che Mundugwao akitoa mchango wake kuhusu shindano la BSS wakati wa kikao hicho cha Tathimini ya shindano hilo.
Che Mundugwao akiwa katika picha ya pamoja na washindi wa BSS kwa mwaka 2011 Hadj Ramadhan (Kushoto) na Waziri Salum.
Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wasanii waliotoka katika programu ya kusaka vipaji vya muziki ya Bongo Star Search kuwa na mikakati ya kujiendeleza wenyewe ili kufikia kilele cha mafanikio.
Wito huo ulitolewa jana na mratibu wa BSS kutoka BASATA Vicky Temu wakati akichangia katika kikao cha tathimini ya shindano hilo kilichofanyika Ukumbi wa BASATA mapema wiki hii.
Vicky alisema kuwa, wasanii hao wanatakiwa kutambua kuwa uhusiano kati yao na shindano la BSS unalindwa na kusimamiwa na mikataba wanayotiliana saini toka wanapoingia kwenye shindano hilo hivyo inapofikia ukomo hawana budi kujipanga kwa ajili ya kujiendeleza kisanaa.
“Wasanii wanaoshiriki BSS wanapaswa kuwa na mikakati ya kujiendeleza baada kuwa wametambuliwa.Shindano hili linawaibua kutoka chini hivyo lazima kuwe na daraja linalowafanya wajiendeleze kisanaa” alisisitiza Bi. Temu.
Hata hivyo, wadau waliochangia kwenye tathimini hiyo walimtaka mwandaaji wa shindano hilo Ritha Paulsen kuangalia namna ya kujenga daraja la kuendeleza vipaji vinavyokuwa vimepatikana kwani wengi wao wanatoka mikoani na hivyo kukosa mbinu za kuingia kwenye soko la muziki.
Walimshauri awe na utaratibu wa kuwaandalia semina na kozi fupifupi washiriki wa shindano hilo zitakazolenga kuwaandaa kuingia kwenye soko la muziki lakini pia kuwa wajasiliamali wazuri katika Sanaa.
“Washiriki wa BSS wanapokuwa kwenye kambi waandaliwe vema kuingia kwenye soko la muziki. Wengi wao wanakosa mbinu na mikakati ya kuliteka soko kutokana na kutoka mikoani hivyo wasaidiwe na wapewe mafunzo au elimu katika eneo hili” alishauri Mjumbe.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Matukio kutoka BASATA, Malimi Mashili aliwataka waandaaji wa BSS kuhakikisha wanatekeleza maagizo mbalimbali waliyopewa kwa ajili ya kupatiwa kibali cha kuendesha shindano hilo mwaka huu.
Maagizo waliyopewa waandaaji hao ni pamoja na; kuwa na bajeti kamili ya shindano hilo, kuwekwa wazi kwa zawadi za washindi, kuwepo kwa mikataba baina ya washiriki na BSS, kuwasilisha majina ya majaji wa shindano hilo, uwezo wa BSS kuendesha shindano hilo na maagizo mengine.
Akizungumza kwenye tathimini hiyo, Mwandaaji wa shindano hilo Ritha Paulsen alisema kuwa, shindano hilo limekuwa likimgharimu fedha nyingi lakini kwa kuwa limejikita kwenye kuinua vipaji vya wasanii wachanga na anapenda kusaidia analazimika kufanya.
“Shindano hili tunalifanya kwa gharama kubwa sana lakini tunajitahidi kusaidia wasanii wetu ili wafahamike na baadaye wajisimamie katika kazi zao” alisisitiza Ritha.
Aliongeza kuwa, BSS imekuwa ikijitahidi kusaidia wasanii katika kurekodi na kujiendeleza lakini changamoto kubwa imekuwa kwa vyombo vya habari na wakuzaji sanaa (mapromota) kuwapokea wasanii hawa kutokana na kukithiri kwa vitendo vya rushwa na mtizamo hasi kuwa, wasanii wanaotoka BSS wanakuwa na fedha nyingi.
Kuhusu maagizo aliyopewa na BASATA aliahidi kuyafanyia kazi ilil kupewa kibali cha mwaka huu kwa ajili ya mchakato wa shindano hilo kuanza mapema wiki hii.