Thursday, June 21, 2012

" Dogo, Hebu Sikiliza Kwanza!"
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi akizungumza na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika katika viwanja vya bunge jana.
 Mnyika amerejea kuhudhuria vikao vya bunge baada ya juzi kutimuliwa bungeni na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai. Picha na Edwin Mjwahuzi

MWASISI wa Chadema, Edwin Mtei amemtetea Mbunge wa Ubungo, John Myika kuwa alikuwa sahihi kusema kwa Rais Jakaya Kikwete ni dhaifu, kwa kuwa kuna matukio mengi yaliyohitaji uamuzi wake na hakuutoa kwa wakati.


Pia Mtei amelaumu Kanuni za Bunge zilizomwezesha Naibu Spika, Job Ndugai kumtoa nje ya ukumbi wa Bunge mbunge huyo.


Juzi, Mnyika alitolewa nje ya ukumbi wa Bunge, baada ya kukukataa kufuta kauli yake kuwa ‘Rais Jakaya Kikwete ni dhaifu’.
Akitetea kauli hiyo, Mtei alirejea baadhi ya matukio aliyodai yanaonyesha udhaifu huo, ukiwamo uamuzi ya Rais Kikwete juu ya hatua za kuwachukulia walioiba fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).


Mtei alifafanua kwamba, kitendo cha Rais Kikwete kuwataka wezi hao warudishe fedha walizoiba badala ya kuwakamata, kinadhihirisha udhaifu mkubwa wa kiongozi huyo.


“Rais Kikwete ana udhaifu wa kuwachukulia hatua za kisheria watu ambao wanahujumu taifa kwa ufisadi…udhaifu wa Rais ni kama kutowadhibiti wezi wa fedha zetu kama fedha za EPA. Aliwaambia wezi warudishe fedha, badala ya kuwatia ndani wanabaki wanatamba kwa kuiba fedha zetu,” alisisitiza Mtei aliyewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu.


Alisema kibaya zaidi ni kwamba, nchi inayumba kutokana na uongozi mbovu kuanzia ngazi ya urais hadi chini, kwa kuwa tunaongozwa na watu wasiojua na kuisimamia Katiba.
Chanzo. mwananchi. http://www.mwananchi.co.tz