Sunday, June 24, 2012

Duke Gervalius : vyombo vya habari havisaidii kukuza sanaa yetu.KATIKA mambo ambayo prodyuza Duke Gervalius anayaamini na kuyafuata ni kujali kile alichoifikishia jamii yake hasa katika upande wa Elimu na masuala ya kiburudani.

Duke kutoka lebo ya Music Lab maarufu kama M Lab, ni kati ya maprodyuza wachache nchini Tanzania waliodhamiria kuhakikisha kwamba wanayafikia malengo waliyojiwekea, huku wakihakikisha kuibadili jamii ya sasa kutoka katika uelewa duni.

"Nikikuletea maji wakati una kiu, sidhani kama utakataa kuyanywa kwa sababu humjui aliyekuletea, hivyo naamini hakuna kitu ambacho kitamnufaisha mwanajamii iwapo  nikaanza kuyaelezea maisha yangu, bali najua nifanye nini kwa ajili ya jamii yangu ili inufaike" anasisitiza.

Anasema wingi wa baadhi ya mambo yasiyo na ulazima ni mojawapo ya kikwazo kikubwa katika maendeleo ya tasnia ya muziki Tanzania.

Kulingana na wingi wa vyombo vya habari hapa nchini na upande wa sanaa na wasanii kupata nafasi kubwa katika vyombo vya habari, Duke anavilaumu vyombo vya habari kwa kuwa  mojawapo ya kikwazo katika tasnia hii, kutokana na kurudia mara kwa mara mambo yenye ufanano.

"Kwa kutambua kwako kwamba tasnia hii imekwama sehemu moja kwa muda mrefu bila mabadiliko yatakayo sababisha kuendelea mbele, mfumo wa mahojiano mengi katika vyombo vingi vya habari nchini kuhusiana na wahusika wa tasnia ya sanaa kwa ujumla (wasanii, watayarishaji na waigizaji) ni yale yale tangu wahusika hawa waanze kuhusishwa na vyombo vya habari kwa upande wa mahojiano" anasema.

Kwa upande wa maendeleo ya sekta ya sanaa Duke anasema serikali imelenga sekta ya sanaa katika bajeti yake kwa mwaka 2012/2013, lakini bado hadhani katika baadhi ya mambo waliyoyazungumzia yatamnufaisha mtayarishaji kwani amesahaulika.

"Kila palipo na faida hapakosi kuwa na hasara, swala ni wingi wa faida au hasara kwa kuzingatia misingi husika. Serikali imezungumzia vitu vingi kuhusu mlengo wao kwa sanaa, sasa kabla ya kuwaza faida napenda kuanza na msingi kwa maana ya mtaji unaopelekea faida.

"Je? sheria inazungumzaje juu ya mtayarishaji wa ala za muziki na ina nafasi ipi kwa mtayarishaji? Inajukumu lipi katika ulinzi wa haki ya mtayarishaji? Je? ni kweli tunahitaji yaliyozungumzwa na serikali ili kutatua tatizo?

"Sidhani kama ni sahihi kuhangaikia ufumbuzi wa tatizo pekee pasipo kujali sababu inayopelekea kuwepo kwa tatizo" anasema Duke.

Prodyuza Duke alianza kufanya kazi ya kutayarisha muziki mwaka 1998. Mwaka 2004 baada ya studio kuanzishwa ambayo ilikua ikiitwa Pinnacle Production wakiwa na prodyuza kutoka kenya Dunga, na wakafanikiwa kufanya kazi kama

Usipime ya Black Rhinno, Temba Ft Ray C – Nipe Mimi, Profesa ft Bamboo – Karibu, Chegge ft Temba – Hili Dude na nyingine nyingi.

Duke hakuishia hapo tu mwaka 2005-2008 akatoka Pinnacle Production na akaamua kuwa prodyuza wa kujitegemea na alifanikiwa kufanya kazi na Studio mbali mbali kama 41 records, Kama Kawa Records, Pasu kwa Pasu records, Dhahabu Records, Bongo Records & Tongwe Records

 Ambapo alifanikiwa kufanya nyimbo ya Wanaume halisi – tatu bila Remix, I am Proffesinal ya Fid Q, Zero – Witness ft Fid Q, O-ten ft Chidi – Nyandindi, Chiku Ketto ft Lameck Ditto – Muda Umefika, Ripoti za Mtaani Fid Q ft Zahiri Zorro, Traveller ya Solo Thang, Babuu wa kitaa – Wa Kitaa.

Duke pia alifanikiwa kufanya Mixtape Kitaani Vol 1 ambayo ilikua na collection ya baadhi ya nyimbo ambazo aliwahi kufanya akiwa kwenye studio mbali mbali.

mwaka 2009 Duke alianzisha Studio, Music Laboratory (M Lab, Music Lab) ambayo akiwa hapo alifanikiwa kutengeneza nyimbo kama Wimbo – Grace Matata, Kila Siku, Nicki Mbishi ft Godzilla, One, Belle9, The Incredible ya One ft Stereo, Chidi Beenz, Izzo B, Free Soul – Grace matata, Ben Pol – Nikikupata na Napata Raha zote zikiwa za Ben Pol, Punch line ya Nicki Mbishi, Robo Saa ya Amini, Wrong Sms ya Barnaba na Lina, Atatamani ya Lina.

Pamoja na hao, bado kuna idadi kubwa sana ya wasanii ambao wamefanya kazi na Duke na mpaka sasa. Bila shaka huyu ndio Duke  ambaye ulikuwa humfahamu na haya ni machache kati ya mengi ambayo ameifanyia jamii yake katika ulimwengu wa sanaa na burudani.