Wednesday, June 27, 2012

LULU: BADO NATESEKA

                                                                                                                                                      
Stori: Richard Bukos
MSANII wa filamu Bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ juzi Jumatatu aliwaambia ndugu zake kuwa bado anateseka baada ya kesi yake inayomkabili ya kuhusishwa na kifo cha msanii mwenzake, Steven Kanumba kupigwa kalenda baada ya suala lake kuhusu umri wake kuamriwa kupelekwa Mahakama ya Rufaa Tanzania.
Muda mfupi baada ya uamuzi huo uliofikiwa Mahakama Kuu mbele ya Jaji Twalib Fauz anayesikiliza kesi hiyo na Lulu kutolewa katika chumba cha mahakama tayari kwa kurudishwa rumande, msanii huyo aligonganisha macho na mmoja wa ndugu zake huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Bado nateseka,” alisema Lulu bila kuongeza neno lingine hali iliyozua majonzi mazito kwa ndugu yake huyo.
Lulu (pichani) alifikishwa katika Makahama Kuu ya Tanzania ambapo kesi yake ilitajwa tena mbele ya Jaji Fauz kwa lengo la upande wa utetezi kuwasilisha vielelezo vya kuthibitisha umri wake ambapo unadai hajafikisha miaka 18.
UTETEZI WAKWAMA TENA
Hata hivyo, upande wa utetezi ukiwa tayari kuwasilisha vielelezo vyao, Jaji Fauz alimtaka Wakili wa Serikali, Elizabeth Kaganda kuzungumza lolote kabla mawakili wa Lulu kutoa vithibitisho vyao kama ushahidi.
Wakili Kaganda aliibua hoja mpya ya kupinga vielelezo hivyo kutolewa mahakamani hapo na kusema wameshapeleka hati ya rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa kupinga kujadili upya umri wa msanii huyo mahakamani hapo.
Awali wakiwa mahakamani hapo, mawakili wa pande zote walifikia muafaka wa kuujalidi upya umri wa msanii huyo ambapo serikali ilipeleka vielelezo vya umri wa Lulu kuwa ni miaka 18.
Hata hivyo, juzi upande huo wa Jamhuri uliomba kusitishwa kwa zoezi hilo baada ya kukata rufaa ili uendelee kutambulika kuwa ni miaka 18 aliouandikisha msanii huyo na kutia saini yake alipokuwa akihojiwa kituo cha polisi baada ya kukamatwa kuhusu kesi hiyo.
Kufuatia ombi hilo hilo la rufaa, mawakili wa Lulu, Kennedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgency Massawe waliushutumu upande wa Jamhuri kwa kuwasumbua na kuwa vigeugeu kwani wao ndiyo walioomba kesi hiyo itolewe Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kupelekwa mahakamani hapo kwa ajili ya kujadili umri.
Jaji Fauz aliipitia nakala ya barua iliyopelekwa Mahakama ya Rufaa na mawakili wa serikali na kutoa uamuzi kuwa kesi hiyo ipelekwe Mahakama ya Rufaa kwa ajili ya kutolewa upya uamuzi wa kujadili umri wa msanii huyo.

DK. CHENI AWATENGANISHA WAZAZI WAKE
Katika hali ya kushangaza, wazazi wa Lulu, hawakukaa pamoja, msanii wa filamu, Mahsein Awadh ‘Dk. Cheni’ ndiye aliyekaa katikati yao.
Jambo lililozidisha huzuni mahakamani hapo ni mdogo wake ambaye jina lake halikupatikana mara moja, kupelekwa kumsamilia sehemu aliyokuwa amekaa huku akiwa amezungukwa na maaskari magereza.
Hali hiyo ilimfanya Lulu amwage machozi kwa uchungu.
Kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Julai 09, mwaka huu kabla ya kuhamishiwa Mahakama ya Rufaa.