Wednesday, June 27, 2012

TAARIFA KUTOKA CHADEMA: RADA,Fedha Uswisi,CHADEMA na Orodha ya Mafisadi


 Mbungea wa Jimbo la Ubungo(CHADEMA)na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi,Mheshimiwa John Mnyika
--
 Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinarudia kutoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete kutumia mamlaka yake ya kikatiba kuagiza kukamatwa kwa watuhumiwa wote wa ufisadi wa RADA ambao CHADEMA imewataja kwa nyakati mbalimbali ikiwemo katika orodha ya mafisadi (list of shame) tarehe 15 Septemba 2007 katika Uwanja wa Mwembeyanga. CHADEMA kinatambua kwamba kuachwa kwa mafisadi bila kuchukuliwa hatua kamili za kisheria na mali zao kufilisiwa kunafanya taifa kuendelea na fisadi ikiwemo ule wa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), Richmond na sasa tuhuma mpya za ufisadi kwamba kuna vigogo wenye kiasi cha bilioni 303 kwenye akaunti Uswisi ambazo zinadaiwa kuwekwa na makampuni ya madini, mafuta na gesi asili. Kutokana na sheria za usiri za Uswisi; CHADEMA kinaitaka Serikali inayoongozwa na CCM kuwasiliana na Serikali ya nchi hiyo ili kuanza mchakato wa kuwezesha mahakama za nchi hiyo kutoa ruhusa kutolewa kwa taarifa zote kuhusu wenye akaunti hizo na makampuni yaliyoweka kiasi hicho cha fedha ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa Sheria za Tanzania na Sheria za Kimataifa. Izingatiwe pia kwenye orodha ya mafisadi CHADEMA iliwataja pia kwa majina viongozi wa serikali ambao waliingia mikataba ya kifisadi ya madini na rasilimali nyingine za taifa; kutolewa kwa taarifa hizo za benki za nje kutathibitisha ukweli na pia kubainisha watuhumiwa wengine zaidi. Wakati huo huo; CHADEMA kinaitaka Serikali inayoongozwa na CCM kuzingatia mpango kati yake na Serikali ya Uingereza kupanga matumizi ya fedha kiasi cha Tshs. 72.3 billioni za RADA zilizorejeshwa baada ya kubainika zilizochotwa kifisadi na Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza. CHADEMA kimeshangazwa na uamuzi wa serikali inayoongozwa na CCM kubadilisha mpango wa kujenga nyumba za walimu; kinyume na mpango huo wakati huu ambapo serikali iko katika mgogoro na walimu kutokana na kutowatimizia madai yao ya msingi ikiwemo nyongeza ya mishahara, kulipa madeni na kupunguza kodi kwenye mishahara. CHADEMA inaitaka serikali kukumbuka kwamba mpango huo ulikuwa moja ya ushahidi muhimu uliotolewa Mahakamani kumshawishi Jaji kutoa uamuzi wa kuridhia makubaliano kati ya SFO na BAE kwamba fedha hizo zingetumika Kununua vitabu 4.4 milioni kwa ajili ya wanafunzi, vitabu 192,000 Kwa ajili ya walimu kufundishia, madawati 200,000, kujenga nyumba 1,196 za walimu wa shule za msingi vijijini, kujenga vyoo 200,000 kwenye shule za msingi. CHADEMA imeguswa pia na taarifa kwamba zabuni ya kuchapa vitabu hivyo imetolewa kwa kampuni ya Kampuni ya Kiingereza ya Oxford University Press hali ambayo itafanya sehemu kubwa ya fedha hizo kurejea huko huko Uingereza; hivyo CHADEMA inaitaka serikali kuweka mfumo wa kuhakikisha fedha hizo kwa sehemu kubwa zinatumiwa katika viwanda vya uchapishaji vya hapa nchini ili kuchangia katika uchumi wa nchi. Imetolewa na: John Mnyika (Mb) Mkurugenzi wa Habari na Uenezi 25 Juni 2012