Wednesday, June 27, 2012

Mwenyekiti wa Jumuiya ya madaktari nchini atekwa na kuumizwa vibayaDr. Ulimboka

Kituo cha ITV kupitia Twitter kimesema mwenyekiti wa jumuiya ya madakatari Dr. Stephen Ulimboka ametekwa na kupigwa na watu wasiojulikana na anapelekwa katika hospitali ya mifupa ya Moi.


Kwa mujibu wa mtandao wa Jamii Forums Dr. Ulimboka ametekwa majira ya saa sita usiku na watu watatu waliokuwa na silaha za moto na kumpeleka kusikojulikana! Inasemekana alipigiwa simu na jamaa mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la 'Abeid' ambaye tangu mwanzo amekuwa akiwasiliana naye na kujiita afisa wa serikali na kudai kuwa alitaka aonane naye face to face kwa ajili ya mazungumzo.

Dokta huyo aliokotwa akiwa na hali mbaya sana na hawezi kuzungumza.

Tukio hilo limetokea wakati kumekuwepo na mgomo wa madaktari nchi nzima ambao hata hivyo wameonekana kusalitiana kwa kutokuwa na msimamo wa pamoja, kwani maeneo mengine yote huduma zimeendelea kama kawaida, isipokuwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Madaktari hao wametangaza mgomo usio na kikomo kwa lengo la kuishinikiza serikali kutimiza mahitaji yao, ikiwemo kuboresha mazingira ya kufanyia kazi pamoja na kuwapandishia mishahara.

Licha ya mgomo huo kuanza kuleta madhara kwa wagonjwa katika siku ya kwanza juzi, kwa madaktari kutofanya kazi katika hospitali mbalimbali nchini, jana hali hiyo ilikuwa tofauti kwani sehemu nyingi huduma ziliendelea kutolewa kama kawaida.
Source: Ipp Media