Saturday, June 30, 2012

TAASISI YA MASHEIKH NA WANAZUONI WA KIISLAMU TANZANIA YAUNGA MKONO KAULI YA MUFTI, YASEMA HAIONI TATIZO LA SENSA YA WATU NA MAKAZI 2012


Sheikh Hamis Mattaka(kushoto) akitoa tamko mbele ya waandishi wa habari kwa niaba ya Mwenyekiti wa jopo la Masheikh wanazuoni wa kiislam Tanzania kuhusu mchakato wa kukusanya maoni ya Katiba, Sensa ya watu na Makazi na Hali ya Zanzbar leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Sheikh Iddi Simba.


Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Dar es Salaam.
Taasisi ya masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania imeunga mkono kauli iliyotolewa hivi karibuni na Sheikh mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban Simba ya kuwataka waislamu na watanzania kote nchini kushiriki kikamilifu katika Sensa ya watu na Makazi itakayofanyika Agosti 26 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kwa niaba ya mwenyekiti wa jopo la masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania Sheikh Hamis Mattaka amesema hatua hiyo inafuatia kuwepo kwa baadhi ya makundi yanayowahamasisha waumini wa dini ya kiislamu na wananchi kutoshirika zoezi la Sensa ya watu na makazi.
Amesema wao kama jopo la wanazuoni hawaoni tatizo la zoezi hilo kutokana na umuhimu wake kwa taifa na kuongeza kuwa Sensa ya watu na makazi ipo kwa mujibu wa sheria za nchi na imepitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jopo hilo limeiomba serikali kuweka sheria itakayozuia utoaji wa takwimu zinazohusu dini za watanzania zinazotolewa na vyanzo mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa kuwa kipengele hicho si sehemu ya sensa nchini.
“Tunajua kuwa serikali ilikua na nia njema kukiondoa kipengele cha dini katika Sensa hapana budi nia njema hiyo ya serikali ilindwe kwa kuweka sheria itakayozuia kutoa takwimu zinazohusu dini za watanzania” amesema Sheikh Mattaka.
Amefafanua kuwa Sensa ya awali ya mwaka 1957 kipengele cha dini kilihusishwa na baadaye kuondolewa katika Sensa zilizofuata kwenye madodoso ya kukusanyia takwimu za kaya.

“Sisi kama jopo kila siku tunasema ili twende salama kama wananchi wa nchi hii ni wajibu wetu kuheshimu na kufuata sheria kwa maana ya kutii sheria bila shuruti, kwa hiyo tunasema Sensa ya watu na makazi ni jambo la kisheria si jambo la mitaani, hatuwezi kulumbana na kujadili jambo ambalo liko wazi kisheria na limepitishwa na wabunge tuliowachagua sisi wenyewe”
Amefafanua kuwa zoezi la Sensa ya watu na makazi litaiwezesha serikali kupanga mipango ya maendeleo kwa kuwa na takwimu sahihi za watu na makazi, hali ya kipato cha kaya, vizazi na vifo na pia kuiwezesha serikali kwapatia huduma bora wananchi wake.
Katika hatua nyingine jopo la masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania imewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya katiba.
Aidha jopo hilo limewataka watanzania wote kwa ujumla kuitumia fursa hiyo muhimu kutoa maoni ambayo yataiwezesha nchi kupata katiba itakayokidhi matakwa ya wananchi.
“ Sisi kama jopo la wanazuoni wa kiislamu tunawataka waislamu na watanzania wote kwa ujumla kuitumia fursa hii muhimu kwa kutoa maoni yao ili hatimaye nchi yetu ipate katiba itakayokidhi matakwa ya wananchi kwa miaka mingi ijayo” amesema Sheikh Mattaka.