Saturday, June 30, 2012

Waziri Mkuu Ataka Wajasiriamali Wawe Makini


WAZIRI MKUU Mizengo Pinda (pichani) amewataka wajasiriamali wa kati na wadogo nchini wawe waangalifu na makini katika biashara wanazopanga kuzifanya kama kweli wanataka kufanikiwa maishani na akawaonya wale waliopata mbegu mtaji kuchukua tahadhari zaidi.

Ametoa onyo hilo leo mchana (Jumamosi, Juni 30, 2012) wakati akizungumza na wajasiriamali kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani ambao walihudhuria sherehe za kutoa zawadi kwa washiriki wa Programu ya Fanikiwa Kibiashara (Business Development Gateway - BDG) kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.“Naomba niwatahadharishe kuwa ujasiriamali unataka umakini wa hali ya juu.

Mmoja wa Wajasiriamali mashuhuri huko Marekani aliwahi kutoa tahadhari kwa kusema:"Business is like oil, it won't mix with anything but Business" akimaanisha kwamba biashara ni kama mafuta ya kulainisha mitambo (oil) ambayo hayachanganywi na kitu kingine chochote, isipokuwa oil yenyewe.
Tunahitaji uangalifu na umakini katika kufanya biashara zetu bila kuchanganya na mambo mengineAmesema mtu anapochukua mkopo kwa nia ya kuanzisha biashara kisha akaamua kuoa mke wa tatu au kununua gari kwa kutumia fedha hiyo ya mtaji ni lazima atakwama kwa sababu atakuwa amechakachua dhima nzima ya ile biashara yake.Alisema katika mabanda ya maonesho aliyotembelea leo, ameona changamoto kuu tatu ambazo zinahitaji kuangaliwa haraka ili kuinua soko la bidhaa za wajasiriamali hao.

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni ukosefu wa vifungashio bora, ukosefu wa alama za viwango kutoka shirika la viwango nchini (TBS) na ukosefu wa alama ya biashara (bar code) katika bidhaa zao. “Bidhaa zenu ni lazima ziwe na vifungashio vizuri vyenye mvuto ili mnunuzi ashawishike kununua.”“Nawasihi mfuate masharti ya shirika la viwango nchini ili bidhaa zenu zikubalike, waoneni wahusika ili mpate bar code kwenye bidhaa zenu. Bidhaa zenu zikiwa na bar code zitakubalika kokote ulimwenguni,” alisisitiza.Waziri Mkuu pia alisema anatatizwa na changamoto moja kuu ambayo ni ya kuhakikisha mpango wa BDG unaendelezwa ili uwanufaishe watu wengi zaidi.
“Mpango huu umefikia mwisho, na umedumu kwa miaka minne tu. Mwenyekiti wa TPSF itabidi tuangalie hata uwezekano wa kukopa ili jambo hili zuri lisiishie hapa,” alisema.“Napata faraja na suala zima la kuendeleza wafanyabiashara wadogo kwa sababu najua wajasiriamali wakiwezeshwa iko siku umaskini wa Watanzania unaweza kutoka kupitia ujasiriamali,” aliongeza.Akizungumza katika sherehe hizo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF), Bi.

Esther Mkwizu alisema jumla ya washindi 1,570 kutoka mikoa yote wamepatiwa tuzo ambayo ni mbegu mtaji yenye thamani ya sh. bilioni 5.75/-.Alisema katika kipindi cha miaka minne ambacho mradi huo wa BDG umekuwa ukiendeshwa hapa nchini, jumla ya sh. bilioni 20 zimeingizwa katika uchumi wa Tanzania kupitia wajasiriamali wadogo wadogo.Naye Makamu Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Uingereza (DfID), Bi. Ros Cooper alisema hakuna nchi yoyote duniani ambayo haihitaji wajasiriamali katika kukuza uchumi wake.
“Wajasiriamali wadogo ndiyo wanaoibua mawazo mapya na ndio wanaoleta ubunifu mpya kila kukicha... tunawahitaji sana na kikubwa ni kuwasaidia ili mawazo yao mapya na ubunifu wao viweze kutimia,” alisema.Alisema Serikali ya Uingereza itaendelea kufanya mazungumzo na TSPF ili kuona uwezekano wa kuendelea kuifadhili programme ya BDG ambayo inafikia mwisho wake mwaka huu.

Alisema anafarijika mno kwa sababu asilimia 56 ya washiriki wa programme hii ni wanawake na asilimia 43 ya washiriki ni vijana walio chini ya miaka 35 lakini kupitia klabu za BDG alizotembelea huko Kilimanjaro na Arusha ameridhishwa na utendaji kazi aliouona.Mapema, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Bw. Godfrey Simbeye alisema wameweza kuwafikia Watanzania mbalimbali katika mikoa yote na kufikisha idadi ya wajasiriamali 8,700 ambao wamerasimisha biashara zao na wote wanatambuliwa walipo, wako tayari kuajiri watu wengine kupitia biashara walizozianzisha.

Alisema changamoto wanayokabiliana nayo kwa sasa ni kutorasimishwa kwa biashara nyingi na kwamba TPSF inapanga kuifanya kuwa elimu ya ujasiriamali inakuwa endelevu.