IKULU ILIINGILIA KESI YA UCHAGUZI. – GODBLESS LEMA.
“ Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi na shukrani nyingi kwa ndugu zetu wa Arusha kwa kuwapokea vizuri na kuwakarimu vyema wageni wetu hao. Nawaomba waendelee na moyo huo mpaka watakapoondoka wote. Naomba kuwepo kwa mkutano huu kuwakumbushe umuhimu wa mji wenu kuwa tulivu. Miaka miwili iliyopita isingekuwa rahisi kwa watu au shirika kubwa la kimataifa kama Benki hii kuamua kufanya mkutano wake Arusha. Isitoshe hata sisi wenyewe tusingeshawishika kuomba au kukubali maombi ya namna hiyo. Lakini sasa imewezekana. Naomba kila mmoja wetu aweke azimio moyoni mwake la kuhakikisha kuwa hali ile haijirudii tena. Nyota ya Geneva ya Afrika lazima iendelee kuangaza. Yaliyopita si ndwele tugange yajayo . ( J.K . KIKWETE.)
“Narudia tena , IKULU iliingilia kesi yangu ya Ubunge”.
Mh Rais nimekusikiliza kwa makini sana ila nakupa pole kwani bado unafikiri unaongea na Tanzania ya mwaka 1961 , umesema sasa Arusha ni shwari tofauti na miaka miwili iliyopita kwani sasa kuna amani na utulivu wa kutosha ndio maana hata mkutano wa AFDB umefanyika Arusha .
Mh Rais , najua IKULU iliingilia kesi yangu kama ilivyoonekana na ndio sababu hata Mkuu wa Mkoa wa Arusha wakati anaapisha Wakuu wa Wilaya alimpongeza Jaji kwa hukumu nzuri aliyowafurahisha wakati kesi hiyo iko mahakama ya Rufaa , lakini jambo moja la msingi ambalo huwezi kulitambua kwa sasa ni kuwa Haki na Ukweli haviwezi kushindwa na dhuluma, ubaya wala mamlaka , natambua wewe ni Rais na unayo mamalaka makubwa katika Taifa hili lakini vile vile nataka utambue kuwa huna mamlaka makubwa dhidi ya haki , utu na ukweli.
Mh Rais hakuna Amani Duniani inayozidi Haki na usawa ,utu na ukweli , haipo na wala haitakuwepo , ndio maana kila siku nasema ni “Afadhali Vita Inayotafuta Haki na usawa kuliko Amani inayopumbaza na kudhalilisha utu wa Mwanadamu “ umefurahia sana mkutano uliokupa fursa ya kutoa maneno ya kebehi na kudhihirisha ila chafu iliyofanywa na Serikali yako na kujaribu kuhadaa Umma kama ilivyo kawaida ya Serikali yako na Chama chako , hata hivyo wakati huu kuna mambo ya msingi yakushughulikia zaidi ya kebehi na hadaa , Uchumi wa Nchi umeyumba, huduma za msingi za jamii zimepuuzwa, Mpasuko katika suala la Muungano na vururugu zinazoendelea Zanzibar , mfumuko wa bei hizi ni sababu chache ambazo haziwezi kuruhusu wakati huu kuwa wakati wa kebehi na mizaha isipokuwa kazi .
Mh Rais , Mama Theresa , Nelson Mandela , Martin Luther Jr na Malcom X hawakuwa Wabunge kupigania haki za Nchi yao na watu wao , sihitaji Ubunge kupigania ukweli, haki na utu , nahitaji dhamira safi , nia njema na huu utakuwa wajibu wangu mpaka nakwenda kaburini , nitakapomaliza mbio hizi najua nitapata fursa ya kutazama nyuma yangu nione nini nilifanya , ukweli nisingependa kuona vituo vya mafuta , magorofa , magari na viwanja vingi kila kona ya Nchi bali Haki ,Usawa na utu vikiwa kama nguzo ya imani ya watawala wetu watakaokuwepo, pengine sitaishi miaka mingi sana kama utachukizwa sana na waraka wangu huu kwani Polisi , Usalama wa Taifa na Jeshi la Wananchi wanakutii wewe , hata hivyo siogopi kufa kwani nisipokufa kesho , nitakufa siku moja ambayo siijui , napenda kuishi maisha marefu nimwone mke wa mtoto wangu kama itawezekana , lakini kuliko iwezekane kwa kuishi kwa hofu ni bora ishindakane kwa kuthamini haki , kwa hiyo kama utakuwa umekasirika sana , unaweza kufanya jambo lolote baya kwa kutumia mamlaka yako , niko tiyari sio kesho wala leo isipokuwa sasa hivi, najua IKULU imewazulumu watu wa Arusha Mbunge wao.
Mh Rais ninajua wazi njama zote na hasira hizi zinaweza kuwa zimetokana hasa na mkutano tuliokaa Osterbay Dar mimi na wewe kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 hata hivyo sikupuuza maongezi yetu isipokuwa nilichagua kufuata dhamira yangu na wito wangu wa utumishi wa kweli katika Jimbo langu na Nchi yangu.
Mh Rais nimekuelewa na Wananchi wamekuelewa kila mahali , wewe ni Rais unayo mamlaka makubwa na mimi ni mwananchi mamlaka yangu makubwa ni kwa mke wangu tu , sina Polisi wala Usalama wa Taifa lakini nitawaomba wanyonge wafunge na kusali tuone kama mamlaka yako inaweza kushindana na haki na ukweli .
Mh Rais “Mtu anaweza kuzini kwa siri lakini hawezi kuugua ukimwi kwa siri” Serikali na Chama cha Mapinduzi kimepuuza watu na haki zao kwa muda mrefu , lakini wakati umefika ambapo hawatapuuzwa tena hata hivyo kwa kauli yako hii naamnini haiwezi kuwafundisha kazi majaji wa mahakama ya rufaa .
“ ONLY TIME WILL TELL”.
GODBLESS .J. LEMA.