Tuesday, June 19, 2012

ZITTO AICHANA BAJETI


WAZIRI Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe jana aliwasilisha bungeni bajeti mbadala ya Kambi ya Upinzani kwa mwaka wa fedha 2012/2013, huku akibainisha kasoro lukuki katika bajeti ya Serikali ilioyowasilishwa Alhamisi iliyopita.Bajeti ya Zitto ilitanguliwa na hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Ofisi ya Rais – Mipango, Christina Mughwai ambaye pia aliweka wazi kile alichokiita udhaifu wa Serikali katika kuitekeleza mipango yake ya kiuchumi, hali ambayo inasababisha umaskini kwa wananchi.

Hotuba zote mbili, ya Zitto na Lissu, zilisema licha ya Serikali kutangaza kwamba bajeti ya 2011/12 ilikuwa ya kupunguza makali ya maisha, hakukuwa na nafuu yoyote kwa wananchi kwani maisha yameendelea kupanda.

Pamoja na kupendekeza njia kadhaa za kupanua wigo wa mapato ya Serikali, wapinzani wametaka kufanywa kwa ukaguzi wa deni la taifa, ili kubaini chanzo cha Serikali kukopa na kuweka wazi jinsi fedha hizo zilivyotumika hadi kufikia Sh22 trilioni.

Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni katika hotuba yake alisema mapato ya Serikali yanaweza kuongezwa kwa Sh2.885 trilioni, hivyo kupunguza utegemezi wa mikopo ya kibiashara ambayo imekuwa ikiligharimu taifa kiasi kikubwa cha fedha.

Vyanzo vya kodi na kiasi cha fedha kwenye mabano alivyopendekeza ni marekebisho ya kodi za misitu ikiwamo mkaa (Sh130.8 bilioni), Kupunguza misamaha ya kodi, kuzuia ukwepaji kodi na udanganyifu wa biashara ya nje (Sh742.74 bilioni), Mauzo ya hisa za Serikali (Sh415.55 bilioni), Marekebisho ya kodi Sekta ya Madini na asilimia 25 ya Mauzo ya Madini Nje (Sh578.36 bilioni) na Marekebisho ya Kodi na Usimamizi bora wa Mapato Kampuni za Simu (Sh502.26 bilioni).

Mapendekezo mengine ni Marekebisho ya Kodi ya Tozo ya Kuendeleza Stadi (Sh243.52 bilioni), mapato ya wanyamapori (Sh61.64 bilioni), kuondoa msamaha wa ushuru wa mafuta kwa kampuni za madini (Sh44.9 bilioni), Usimamizi wa mapato ya utalii (Sh51.75 bilioni), Kuimarisha biashara Afrika Mashariki (Sh 114.15 bilioni).

Zitto alisema kama wapinzani wangekuwa madarakani wangekusanya kiasi cha Sh15 bilioni sawa na ile ya Serikali, lakini tofauti ni hatua ya kutenga asilimia 35 ya mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupunguza utegemezi wa bajeti kutoka asilimia 42.37 za Serikali hadi asilimia 21.3.

Deni la Taifa

Kuhusu deni la Taifa, mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini (Chadema), alisema Serikali haipaswi kuendelea kukopa, kwani taarifa rasmi za kibenki na ukaguzi wa hesabu zinaonyesha kwamba deni hilo linakua kwa kasi tofauti na maelezo ya Serikali kwamba linahimilika.

“Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonyesha kuwa Deni la Taifa linazidi kuongezeka kwa asilimia 38 kutoka Sh10.5 trilioni mwaka 2009/2010 hadi Sh14.4 trilioni 2010/2011. Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, Deni la Taifa limefikia Sh20.3 trilioni mpaka ilipofika mwezi Machi mwaka 2012,”alisema Zitto na kuongeza:

“Ukisoma taarifa ya Mwezi wa Mei 2012 ya Benki Kuu ya Tanzania, Deni la Taifa sasa limefikia Sh22 trillion. Suala hapa sio ustahmilivu wa Deni kama inavyodai Serikali, bali ni kwamba tunakopa kufanyia nini?”

Alisema hesabu za bajeti ya Serikali ya 2012/13 inayopendekezwa zinaonyesha kwamba Serikali bado ina mpango wa kukopa kwa ajili ya kugharamia matumizi ya kawaida ambayo hayazalishi wala kutozwa kodi.

“Hatutaki mikopo kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya posho, kusafiri, magari n.k. Tuchukue mikopo kuwekeza kwenye miradi itakayokuza uchumi na kuzalisha kodi zaidi,” alisema.

Kuhusu mfumuko wa bei, Zitto alikosoa hatua zinazopendekezwa na Serikali kukabiliana nao, kwamba ni zile zilizoshindwa katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, mwaka huu. kutoka Mwananchi. www.mwananchi.com