Tuesday, July 10, 2012

Dk. Slaa, Mnyika kuhojiwa Polisi


SIKU moja baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Godbles Lema kuishutumu Serikali kuwa inataka kuwaua, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, ameliagiza Jeshi la Polisi nchini, liwahoji viongozi hao.
Alisema amelazimika kufanya hivyo, ili kupata ukweli wa kilichosemwa na viongozi hao, wakiongozwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.

Dk. Nchimbi, aliyasema hayo jana mjini hapa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

“Ndugu waandishi wa habari, nimewaita hapa ili tuzungumzie suala moja kubwa ambalo lilizungumzwa jana na viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe.

“Katika mazungumzo yake kwa waandishi wa habari, Mbowe alisema Usalama wa Taifa wana mpango wa kuwaangamiza kwa sumu au kwa ujambazi baadhi ya viongozi wa chama hicho.

“Mbowe alisema pamoja na vitisho hivyo, bado hawajatoa taarifa hizo polisi kwa sababu hawaliamini Jeshi la Polisi.

“Kwa hiyo, sisi kama Serikali tumelitafakari hili kwa sababu suala la ulinzi wa wananchi siyo hiari, bali ni suala la wajibu wa kikatiba na kisheria.

“Kwa hiyo, tunapozungumzia usalama wa raia, vyombo vyetu havitamuomba mtu ruhusa kumlinda kwa sababu ni wajibu na kazi yetu kuwalinda Watanzania, tunawataka Watanzania kutosita kutoa taarifa za vitisho katika vyombo vya dola.

“Nichukue fursa hii kuwataka viongozi wote wa kisiasa kutoa taarifa katika vyombo vinavyohusika, hasa polisi, kwa sababu hiyo ni moja ya majukumu yao kikatiba.

“Kwa hiyo, ili kupata uhakika wa taarifa hizi, nimeliagiza Jeshi la Polisi, liwahoji hao wanaosema wanataka kuuawa, waeleze nani anawatisha kisha hatua zichukuliwe,” alisema Dk. Nchimbi.

Katika mazungumzo yake, Waziri Nchimbi alikemea tabia ya viongozi wa kisiasa kuishutumu Serikali hadharani badala ya kupeleka malalamiko yao polisi ili yakafanyiwe kazi.

“Tabia inayoanza kujengeka sasa ya viongozi kupiga kelele nje ya utaratibu ni tabia isiyokubalika, kwa sababu inadhamiria kujenga hofu miongoni mwa Watanzania na inawafanya Watanzania wasiamini vyombo vyao vinavyowalinda kwa mujibu wa Katiba na Sheria.

“Lakini vile vile kuimarisha umaarufu wa kisiasa, bila sababu za msingi ni jambo la kweli kwa mwanasiasa kukubalika katika jamii, lakini kukubalika kwa utaratibu huu, hatuwezi kuukubali.

“Kama Serikali nayo ingekuwa inataka kukubalika kwa wananchi kwa njia za ovyo kama wanazotumia Chadema, basi nayo ingefanya hivyo, lakini hatuwezi kufanya hivyo kwa sababu hakuna sababu za msingi,” alisema.

Dk. Nchimbi alitolea mfano wa tukio la viongozi wa Chadema kuhusishwa na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, ambapo alisema vyombo vya dola havikukurupuka kuwakamata ama kuwapeleka mahakamani viongozi wa Chadema, ingawa walikuwa watuhumiwa namba moja.

“Chadema hawaviamini vyombo vya dola, lakini ieleweke dola inafanya kazi kwa utaratibu na kwa kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio husika.

“Kwa mfano, katika lile tukio la kifo cha Chacha Wangwe, Chadema walikuwa ni kati ya watuhumiwa, lakini hatukuwakamata, polisi walifanya uchunguzi mwishowe dereva wa Chacha Wangwe akakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Juzi, Mbowe na viongozi waandamizi wa Chadema, walizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kueleza jinsi maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa wanavyotaka kuwaua baadhi ya viongozi hao.

Katika mkutano huo, Dk. Slaa, Mnyika na Lema, walieleza jinsi wanavyowindwa na kwamba hawatarudi nyuma katika kuwatetea Watanzania.