Tuesday, July 10, 2012

Kiongozi wa Chama cha Madaktari akamatwaNamala Mkopi
      *Ni Rais wa MAT Dk. Namala Mkopi
      *Kufikishwa Mahakama ya Kisutu leo
      *Wapeleka barua Umoja wa Mataifa
      *Wataka Dk. Stephen Ulimboka alindwe


    JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limemshikilia na kumuhoji  kwa    saa   kadhaa, Rais wa Chama Cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Namala Mkopi    kutokana na agizo la mahakama. Akithibitisha kukamatwa kwa kiongozi huyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi alisema alikiri jeshi hilo kumshikilia Mkopi na kufanya naye mahojiano.

Alisema baada ya mahojiano ya saa kadhaa, jeshi hilo liliamua kumwachia kwa dhamana na kutakiwa kuripoti leo.

Msangi, ambaye pia ni Mkuu wa Upelelezi wa Makosa wa Kanda hiyo, aliimbia MTANZANIA kwa njia ya simu jana kuwa, jeshi la polisi halikutumia nguvu kumkamata Dk. Mkopi, badala yake lilimpigia simu na kumtaka kufika kituoni kwa mahojiano maalum.

“Ni kweli tulimshikilia kwa saa kadhaa Dk. Namala Mkopi na baada ya mahojiano, tulimwachia na kumtaka arejea tena kesho (leo), kituoni kwa hatua zaidi.

“Na yeye mwenyewe, baada ya kupigiwa simu alikuja na kubwa tulilofanya ni mahojiano na kama ni hatua zingine za kimahakama zitafuata,” alisema Msangi.

MTANZANIA ilipomuuliza kama leo kiongozi huyo wa madaktari anaweza kufikishwa mahakamani ama laa, Kamanda Msangi alisema suala hilo litajulikana leo.

“Tumefanya mahojiano naye na masuala yote unayotaka kuniuliza hapa, ninakuomba kuwa na uvumilivu ndugu yangu kesho (leo), tutaweka wazi kila kitu kwani hivi sasa ninaelekea uwanja wa ndege kuna ugeni wa kitaifa na ninalazimika kuwa huko,” alisema Kamanda Msangi.

Wakati huo huo, Chama cha Madaktari Tanzania ( MAT), kimepeleka taarifa Umoja wa Mataifa (UN), pamoja na mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu ya kitaifa na kimataifa, juu ya kuhofia usalama na uhai wa Rais wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka.

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari mjini Dar es Salaam na kusainiwa na Rais wa Chama hicho, Dk. Mkopi, ilisema kumekuwapo na hali ya vitisho kwa baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Madaktari, akiwemo Dk. Ulimboka ambaye yupo nje ya nchi kwa matibabu.

“Nimeamua kuliweka jambo hili wazi ambapo nimepeleka taarifa hizi kwa Umoja wa Mataifa (UN), pamoja na mashirika ya kitaifa na kimataifa yale ambayo yanafanyakazi ya kutetea haki za binadamu ya Human Right Watch na Amnesty International.

“Mashirika mengine ni pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu( LHRC), SIKIKA Tanzania, TGNP na TAMWA, juu ya usalama na uhai wa Dk. Ulimboka pamoja baadhi ya wajumbe wa Jumuiya ya Madaktari.

Aidha barua hiyo, imeutaka Umoja wa Mataifa, kuhakikisha usalama wa Dk. Ulimboka katika hospitali aliyolazwa huko nje.

Ombi lingine la MALT kwa UN wameutaka Umoja wa Mataifa kuwahakikishia usalama viongozi wa Jumuiya ya Madaktari nchini.

Kadhalika wametaka mhimili wa sheria, yaani mahakama ishauriwe kutotumika kwa manufaa ya kisiasa.

Taarifa hiyo, imelitaka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, likumbushwe wajibu wake katika kuibana Serikali kwa vifo na maumivu wanayopata Watanzaniaia kutokana na mgomo unaoendelea.

Taarifa hiyo, ilisema wanapokea ushauri kutoka kwa wanaharakati wa kimataifa namna ya kuweza kuondokana na mgogoro huo.

Kutokana mgomo huo ambao ulitangazwa na Chama cha Madaktari nchini (MAT) na kutakiwa kufanyika Juni 23, mwaka huu ulizuiwa na mahakama Kuu kitengo cha kazi na kumtaka kuiongozi huyo wa madaktari nchini kutangaza kutokuwepo kwa mgomo.

Amri hiyo ya Mahakama imetolewa kukutokana na maombi namba 73 ya 2012 yaliyowasilishwa chini ya hati ya dharura na Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT).

Hata hivyo, wizara ililazimika kuwaandika barua madaktari hao na kuwafikisha mbele ya Baraza la Madaktari Tanganyika kwa hatua zaidi ili iwachunguze na kuamua hatima yao kitaaluma.