Sunday, July 15, 2012

Dongo Janja Chipukizi anayekubaliwa na wengi

 


DOGO Janja, ni msanii chipukizi ambaye kwa muda mfupi amefanikiwa kuteka hisia za wapenzi wengi wa muziki wa kizazi kipya nchini.
Jina lake halisi ni Abdulaziz Chende, kutoka Arusha, kipaji chake kilivumbuliwa na kiongozi wa kundi la Tip Top Connection, Madee alipokuwa katika moja ya matamasha
Baada ya kushawishika na uwezo wa Dogo Janja, Madee alimleta Jijini Dar es salaam kwa lengo la kumuinua zaidi kisanaa na kuchukua jukumu la kumlea ikiwa ni pamoja na kumsimamia masomo yake kwa kumlipia gharama zote.
Hivi karibuni, kulitokea hali ya kutoelewana miongoni  mwa wawili hao hali iliyopelekea msanii huyu kurudishwa nyumbani kwao baada ya Madee kuona kuwa ameshindwa kumlea kutokana na kutozingatia shule na Madee kuamua kumrudisha Dogo Janja nyumbani kwa wazazi wake.
Pande zote mbili kwa nyakati tofauti zimekuwa zikivutana, kila mmoja kumtuhumu mwenzake kuwa ndiye mwenye makosa.
Hata hivyo pamoja na kupenda sana muziki, Dongo Janja anakiri kuwa anaithamini sana elimu na hatapenda muziki uingilie malengo yake kielimu.
Siwezi kuruhusu kitu chochote kiingilie  elimu yangu, ndiyo maana niliumia sana niliposhindwa kufanya mitihani ya kufunga shule  na kurudishwa nyumbani baada ya kupigwa kwa madai ya kutohudhuria shule,”anasema.
Matumaini Mapya
Nyota ya Dongo Janja iliyoonekana kuzama, iliibuliwa tena na Mkurugenzi wa Mtanashati Entertainment, Ostaz Juma Namsoma aliyejitolea kumrudisha jijini Dar es Salaam na kugharamia masomo yake na pia kusimamia kazi zake za muziki.
“Baada ya kupata mfadhili wa kunisomesha nataka niwadhihirishie Watanzania kuwa mie napenda sana shule.” anasema Dongo Janja.
Ostaz kwa upande wake anasema licha ya kuvutiwa na uwezo wa msanii huyo katika muziki, ameamua pia kuhakikisha anapata elimu inayostahili kwani kitendo cha kurudishwa kwao kingeharibu saikolojia yake.
“Kurudishwa nyumbani kungempoteza, si tu kimuziki bali hata elimu yake kwani angeathirika kisaikolojia akiwa bado ana umri mdogo,” anasema na kuongeza:
“Nina hakika kipaji chake kingepotezwa kabisa katika ramani ya muziki, ndiyo maana nikatumia busara kumrudisha ili apate elimu sambamba na kujiendeleza kisanaa.”
 “Watanzania waelewe kuwa kuna vipaji vingi vinapotea kutokana na dhuluma kitu ambacho sikutaka kimtokee Dogo Janja, kama mzazi nitasimamia na kuhakikisha mtoto anapata elimu anayostahili.”anasema.
Dogo Janja alizaliwa Arusha 1997 katika Hospitali ya Mount Meru, alisoma Shule ya Msingi Unga Limited na kuhitimu mwaka 2010. Kwa sasa anasoma kidato cha pili  katika Shule ya Sekondari Makongo, ni miongoni mwa wasanii walioko chini ya kampuni ya Mtanashati Entertainmet.