Friday, July 27, 2012

JD: CHAMELEONE NI TAPELI WA KUTUPWA


John Dilinga, 'DJ JD', nae akiwaeleza wanahabari  jinsi alivyotapeliwa na Chameleone mwaka 2005.
DJ mkongwe nchini, John Dilinga Matlou ‘DJ JD’, leo nae ameweka wazi utapeli aliowahi kufanyiwa miaka saba iliyopita na mwanamuziki raia wa Uganda, mwenye hulka ya utapeli, Joseph Mayanja Chameleone.

JD, amewaeleza waandishi wa habari leo, waliokusanyika kwenye Hoteli ya The Atriums kwamba Chameleone siyo mtu mzuri anapokubaliana na mapromota, kwani hata yeye aliwahi kumtapeli dola za kimarekani 3,000, mwaka 2005.

Alisema mbele ya waandishi wa habari: “Niliwasiliana na Chameleone moja kwa moja, akanikubalia kwenye tamasha langu lililokuwa linaitwa Wakilisha. Nilimlipa dola 3,000, baada ya kupokea fedha, hakuonekana tena na hata simu yangu akawa hapokei.

“Aliendelea kunikimbia hivyo. Tatizo kubwa lipo kwa mapromota wa Kitanzania, hatuna ushirikiano kabisa. Kila alipokuja nchini kufanya shoo, nilimfuata promota husika lakini promota mwenyewe alimficha Chameleone asikamatwe.
“Mwaka 2006, Chameleone alikuja nchini kwenye shoo fulani. Kama kawaida yake alijitahidi sana kujificha nisimfikie. Hata hivyo, pamoja na kujificha kwake, nilipewa taarifa usiku kwamba yupo Bilicanas. Nikawataarifu polisi tukaenda kumkamata.

“Chameleone aliponiaona alinikimbia. Ndugu zangu, Chameleone alikimbia kama mwizi. Pale Bilicanas walikuwepo Rita Paulsen wa BSS na Merey Balhabou. Wakati polisi wamemkamata, Chameleone alikubali namdai dola 3,000 na akakubali kulipa.

“Kusikia hivyo, Rita na Merey wakaniomba nimsamehe kwa sababu mtu mwenyewe amekubali kulipa. Nikawaambia ameshanisumbua sana, Merey akasema kama hatalipa, basi yeye atamlipia. Akanisihi sana kuwa mimi ni mtu wa Morogoro mwenzake, kwa hiyo nimuache Chameleone.

“Nilikubali walichokisema lakini kuanzia hapo, Chameleone na Merey hawakupatikana. Merey alikuwa ‘bize’ na mambo yake, wakati Chameleone hakutaka kupokea simu yangu kabisa.

“Siku moja nilibadilisha namba ya simu nikampigia Chameleone, akapokea vizuri. Nikamkumbusha kuhusu fedha zangu, akaniambia hana uwezo wa kulipa ila anachoweza kufanya ni mimi kuandaa shoo nyingine halafu yeye atakuja ku-perform.

“Pamoja na kuahidi, kila nilipoandaa shoo, ukifika muda wake wa kuja hakufanya hivyo. Hii inamaanisha kuwa Chameleone ana tabia ya utapeli na Watanzania tunapaswa kuwa wamoja kwenye hili tatizo.”

JD alisema, ameamua kutokeza na kueleza haya kipindi hiki ili kila mtu atambue kwamba Chameleone siyo mtu mzuri kwenye fedha na anaweza kumkana promota wakati wowote.