Friday, July 27, 2012

Utafiti wabaini: Wanawake wafupi hatarini kwa vifo vya uzazi


Baadhi ya wanawake wakiwa kwenye wodi ya wazazi ya Hospitali ya Temeke,wakisubiri kujifungua. Picha na Emmanuel Herman
Na Maimuna Kubegeya
SIKU zote mwanamke awapo mjamzito huwa na matarajio makubwa ya kukipata kiumbe chake ambacho huwa ni faraja ya pekee maishani mwake.Lakini inapotokea mwanamke huyo akashindwa kukipakata kiumbe  alichokisubiri kwa hamu kwa muda mrefu wa miezi tisa, huwa ni msiba …  majuto na upweke wa aina yake.
Hiyo ndiyo  hali iwakumbayo wanawake wengi wanaopoteza watoto wao wakati wakujifungua .
Zipo sababu chekwa zisababishazo  vifo vya watoto wachanga na moja ya sababu hizo ni maumbile ya wanawake wenyewe.
Wengine si tu hupoteza vichanga bali hata maisha yao wenyewe huenda yakawekwa rehani katika kipindi hiki.

Kwa mujibu wa Hadija Kimwaga,  Ofisa Muuguzi na Mkunga kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro, wanawake wafupi wako katika hatari ya kupata matatizo wakati wa kujifungua ingawaje si kila mwanamke wa aina hiyo kwani wapo wengine ambao hujifungua kwa njia ya kawaida.
“Baadhi ya wanawake walio na urefu ulio chini ya sentimita 150  huwa na nyonga ndogo. Hivyo, inashauriwa mara watakapokuwa na ujauzito kwenda kwanye vituo vikubwa vya afya ama hospitali kubwa kwani huko wanaweza kupata huduma sahihi”, anaeleza.
Anaongeza kuwa na hii ni miongoni mwa sababu zinazowafanya wataalamu wa afya kuwashauri  kufika kwenye vituo vya afya kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya mtoto na afya zao kwa ujumla katika kipindi hicho.
Kwa wale wanaopata tatizo mara nyingi njia pekee ya kuwanusuru imekuwa ni upasuaji. Hivyo, ikithibitika kuwa nyonga za mwanamke husika hajitanuki kwa kiwango kinachohitajika basi huduma hiyo hutolewa kwa lengo la kunusuru maisha ya mama na mtoto.Lakini hatari kubwa hutokea pale wanapocheleweshwa anasisitiza.
Pamoja na kuwa suala la kimo mara nyingi hutegemea na  hali ya kijenetiki, wakati mwingine ufupi husababishwa na ukosefu wa lishe bora wakati wa utotoni.
Mmoja wa wanawake waliofikwa na msiba wa kupoteza kichanga ni  Margreth Mwenda.

Magreth anasema: “NI siku ambayo siwezi kuisahau maishani kwangu.  Ninakumbuka kuwa ilikuwa mwezi wa Januari mwaka 2000, nikiwa kwenye moja ya kitanda katika wodi  ya wazazi, kwenye  Hospitali ya St. Francis  Wilaya ya Kilombero Mkoa wa Morogoro”, anasemaMwenda.
Kwa wakati huo, kitu pekee alichokuwa akitarajia ni kumkumbatia mwanawe ambaye alikuwa akitarajia kujifungua muda mfupi ujao.
“Huwezi kuamini, mtoto ambaye nilikuwa namsubiri kwa hamu, tena nikimsikia anavyonipiga mateke tumboni, alifariki muda mfupi  kabla ya kujifungua. Alifia njiani,” anasema mwanamke huyu mwanye umri wa makamo.
“Kwani nilishindwa kujifungua kwa njia ya kawaida kutokana na nyonga zangu kushindwa kutanuka. Jambo hilo lilisababisha mtoto kushindwa kushuka kwenye njia yake ya kawaida’’, anafafanua Mwenda.
“Pamoja na uchungu nilionao, lakini naweza kueleza kuwa sababu moja wapo iliyochangia kumpoteza mwanangu, ni kuchelewa kufika hospitalini na hivyo kupoteza damu nyingi sana kabla ya kujifungua”, anasema kwa huzuni mama huyo.
Dk. Hassan Saad kutoka Tume ya Taifa ya Kudhibiti  Ukimwi (Tacaids)anasema  kimo kifupi mara nyingi husababisha matatizo wakati wa kujifungua kutokana tatizo la kushindwa kutanuka kwa nyonga 
Anasema tafiti kadhaa zinaonyesha kuwa mara nyingi lishe duni  wakati wa utotoni hupelekea kudumaa. Jambo linalochangia hupelekea mtoto husika kuwa mfupi.
Baadhi ya mambo yanayochangia hali hiyo ni ukosefu wa vitamini D na ukosefu wa mwanga wa jua wa kutosha unaosababisha kupata matege na magonjwa mengine ya mifupa ikiwamo hilo la kutokuongezeka kwa nyonga.
“Lishe bora ina nafasi kubwa ya kuongeza kimo  na pia kuongeza kimo cha mji wa uzazi” alisema.
Imebainishwa kuwa wanawake walio katika tatizo hili kwa sasa, huwa wameathiriwa wakiwa wadogo.
Dk Maggie Blott, mshauri wa masuala yanayohusu magonjwa ya wanawake, kutoka Uingereza ameandika kwenye mtandao wake kuwa  baadhi ya wanawake walio na kimo kifupi  wana nyonga ndogo, ambazo  hushindwa kushindwa kutanuka wakati wa kujifungua na hivyo  kusababisha madaktari kuchukua uamuzi wa kuwafanyia upasuaji .
“Mara nyingi ili kuokoa maisha ya mama na mtoto, tumekuwa tukitumia njia ya upasuaji”, anaandika daktari huyo.
“ Katika nchi zinazoendelea  umasikini na ukosefu wa lishe bora kwa watoto unasababisha  watoto hao kukua , wakati  mifupa ya wasichana inakuwa haijakomaa.  Hali hii ya kudumaa husababisha matatizo wakati wa kujifungua na pia fistula”, anasisitiza.
Tatizo hili limekuwa ni la kawaida kwa nchi masikini na hasa kwa wanawake na wasichana walio na hali ya chini kimaisha.
Vifo vya wajawazito  mara nyingi vinasababishwa na matatizo wakati wa kujifungua na  vimekuwa vikiongezeka zaidi katika nchi zinazoendelea hasa kutokana na huduma duni za afya zinazotolewa hususani na wakunga jadi.
Wakati mwingine mzazi hupoteza damu nyingi sana kabla ya kujifungua, kutokana na mtoto kukandamiza njia ya uzazi na kusababisha majeraha yanayosababisha kuvuja kwa damu. Jambo linalosababisha mwanamke husika kufanyiwa upasuaji.
Ulaji wa chakula bora tangu kipindi cha mimba na baada ya kuzaliwa, ni njia mojawapo ya kuepuka tatizo hili.
Kwani ikiwa mama atakula chakula bora  wakati wa ujauzito, ni wazi kuwa atajifungua mtoto mwenye afya bora.
Mtoto huyo pia akipata chakula bora wakati wa makuzi yake, ni wazi kuwa atakuwa katika hali bora kiafya. Hali hiyo huchangia kuondoa udumavu, unaopelekea hatari wakati wa kujifungua.
Lakini, kwa wanawake kama  Magreth Mwenda hawana jinsi ya kurekebisha maumbile yao, isipokuwa ni kuhakikisha wanajifungua sehemu salama yenye madaktari wenye ujuzi wa kutosha.
Pia, kuwapa chakula bora watoto wao pindi watakapojifungua ili kuwaepusha na tatizo kama hilo.