Sunday, July 22, 2012

Kuzama Kwa Mv.Skagit Ni Matokeo Ya Kutokutibu Kiini Cha Ajali Iliyopita (Makala, Mwananchi Jumapili)
Na: Maggid Mjengwa,

WATANZANIA tumekumbwa tena na balaa la ajali kubwa ya meli kuzama. Ni wakati sasa wa kujifunza kutokana na yaliyotokea huko nyuma.

Maana ajali ya Mv Skagit inaonekana dhahiri kuchangiwa na uzembe. Na uzembe kwa nchi yetu unalelewa na mfumo mbovu. Na mfumo mbovu unatokana na Katiba mbovu.

Maana, ni katika mazingira haya ya kufanya mambo ya hovyohovyo ndipo tunapokuwa na wanasiasa wa hovyohovyo wenye kuhusika pia na biashara ya uchukuzi na usafirishaji wa abiria.

Ni vigumu kwa mfumo wetu wa sasa, kwa watendaji wa vyombo au taasisi zisizo huru kikatiba na kisheria kuweza kuwasimamia wafanyabiashara dhalimu ambao miongoni mwao wamo baadhi ya wanasiasa wetu.

Tuna lazima sasa kupitia Katiba yetu ijayo, kuvipa nguvu za kisheria vyombo na taasisi zetu muhimu kwa nchi yetu. Tuwe na vyombo na taasisi huru ambazo utendaji wake hauwezi kuingiliwa kirahisi na mamlaka nyingine.

Fikiri leo kama tungekuwa na utaratibu wa kwamba mmiliki wa chombo cha majini au angani na atakayebainika kuingiza nchini chombo kilicho chini ya viwango vinavyokubalika kimataifa na hata chombo hicho kikasababisha ajali ya kuua raia kuwa mmiliki huyo atafungwa jela na kufilisiwa mali zake? Naamini, tungekuwa na vyombo madhubuti na ajali zingetokea kwa bahati mbaya kwa maana yake halisi.

Ni nini basi cha kujifunza kutoka kwenye ajali iliyopita ya Mv Spice Islanders?

Ikumbukwe, Ripoti ya Tume ya kuchunguza ajali ya kuzama kwa Meli ya Mv Spice Islanders ilipendekeza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari, Mustafa Aboud Jumbe pamoja na wahusika wengine wachukuliwe hatua za kisheria na kinidhamu kutokana na uzembe waliofanya na kusababisha kuzama kwa Meli hiyo. Mpaka leo hii hatujasikia adhabu walizopewa wahusika wa ajali ile.

Maana, bado tunakumbuka kuwa, ripoti ile ilibainisha kuwa miongoni mwa watu ambao walibainika na makosa katika ajali ya Mv Spice Islanders ni pamoja na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar, Haji Vuai Ussi, Mkuu wa kituo cha usimamizi wa usalama wa vyombo vya baharini wa Shirika la Bandari, Usawa Khamis Said na Kaimu Mdhibiti wa Bandari ya Malindi, Sarboko Makarani Sarboko.

Wengine ni pamoja na Wanahisa wa Kampuni inayomiliki meli hiyo Jaku Hashim Ayub ambaye ni Mwakilishi na Mbuge wa Jimbo la Muyuni, Salim Said Mohammed, Makame Hasnuu Makame na Yussuf Suleiman Issa.

Alikuwamo pia nahodha wa meli Said Abdallah Kinyanyite na wasaidizi wake, Ofisa usafirishaji wa Shirika la Bandari Hassan Mussa Mwinyi na Mkaguzi wa Meli wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini, Juma Seif Juma.

Ndiyo, wakati bado hatuna hakika ya hatua zipi zilichukuliwa dhidi ya wahusika hawa leo tunaomboleza msiba mwingine kwa taifa.

Hakika, inasikitisha sana, kuwa hata mwaka haujatimu kukumbuka ajali iliyopita ya Septemba 9, 2011, Watanzania tunapatwa na msiba mwingine. Na misiba yote miwili inatokana na uzembe na wala si ya kusingizia ‘Kazi ya Mungu’.

Watanzania sasa tunataka kuona hatua kali za kisheria na kinidhamu zinachukuliwa, tena kwa haraka dhidi ya wahusika waliochangia kwenye ajali ile ya Mv Skagit.

Kwa kuanzia jina la mmiliki wa meli liwekwe hadharani. Na Tume itakayochunguza ajali hii itabaini kuwa mwenye meli ameingiza chombo chakavu, basi, awe wa kwanza kutolewa mfano.

Maana, kama taifa, bila kuwa wakali katika haya ya msingi, basi, tunahatarisha usalama wa taifa letu pia. Kamwe tusiruhusu hilo kutokea. Nahitimisha.
 http://www.mjengwablog.com/