Serikali imeamua kuagiza madaktari kutoka nchi za nje watakaochukua nafasi ya wale wa hapa nchini ambao wamegoma kuanzia mwishoni mwa wiki iliyopita.
Habari kutoka katika moja ya vyanzo vya kuaminika zimesema kuwa uamuzi huo wa serikali ulipitishwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri kilichokutana mjini Dodoma juzi chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilidai kuwa Rais Kikwete alikerwa na tabia ya madaktari kupingana na serikali licha ya juhudi zote zilizofanywa kuboresha maslahi yao.
Kwa mujibu wa habari hizo, kiasi cha sh bilioni 200 kimetengwa kwa ajili ya kuwaleta na kuwagharimia madaktari hao wa nje na pia baraza limepitisha azimio la kuzungumza na hospitali za jeshi kama Lugalo na zingine ndogo kubeba jukumu hilo kwa sasa pamoja kuagiza madaktari wastaafu wote warejee kazini katika kipindi hiki cha mgomo.
Habari zimedai kuwa madaktari hao wanasadikiwa watatoka katika nchi rafiki, zikiwemo India, China, Cuba na Afrika Kusini, na kwamba wataziba kikamilifu pengo la wale wa hapa nchini ambao wamegoma.
Inaelezwa kuwa mara baada aya kukamilika na kuanza rasmi kwa huduma za matibabu, madaktari wa hapa nchini waliomo katika mgomo na wale zaidi ya 200 waliodaiwa kufukuzwa na serikali kimyakimya, watalazimika kurejeshwa kazini kwa masharti makali.
Hata hivyo, uamuzi wa serikali kuwatimua madaktari wakati suala lao liko mahakamani, umewagawa wabunge.
Baadhi ya wabunge walijaribu kuhoji suala hilo Bungeni, lakini walikwama baada ya Spika Anna Makinda kuzuia mjadala huo kwa madai kuwa suala hilo liko mahakamani.
Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamis Kigwangala, alisema kuwa kilichofanywa na serikali ni kiini macho kwani juzi Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema serikali haiwezi kutoa kauli dhidi ya madaktari kwa madai kuwa kuna kesi mahakamani, “Juzi serikali imesema kuwa haiwezi kutoa kauli kwa vile jambo hilo lipo mahakamani, sasa imewezaje kuwafukuza madaktari wakati jambo lipo mahakamani?” alihoji Dkt. Kigwangala.
Aliitaka serikali kuondoa kesi hiyo ili kurejesha majadiliano kwani ndio njia pekee ya kukabiliana na mgogoro huo.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alimshangaa Spika Anna Makinda kuzuia mjadala huo kwani ungeweza kujadiliwa bila kuingilia uhuru wa mahakama.
Juzi uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, uliwafukuza kazi madaktari 229 walioko katika mafunzo kwa njia ya vitendo kutokana na mgomo unaoendelea wa kushinikiza kulipwa posho zao za mwezi mmoja.
Hospitali zingine ambako madaktari wamefukuzwa kutokana na mgomo huo ni pamoja na Mbeya na Dodoma.