Tuesday, July 3, 2012

WASANII JIPANGENI KWA URASIMISHAJI WA SEKTA YA SANAA

Mkuu wa Idara ya Mfuko na Uwezeshaji kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Angelo Luhala (Katikati) akisisitiza jambo wakati akieleza umuhimu wa Wasanii kujisajili ili kuwa tayari kwa ajili ya urasimishaji wa Sekta ya Sanaa. Kulia ni Afisa Habari wa BASATA Aristides Kwizela na Kaimu Mkuu wa kitengo cha matukio BASATA, Malimi Mashili.

Na Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wasanii kujipanga kwa ajili ya zoezi la urasimishaji wa sekta ya Sanaa linalotarajiwa kuanza ifikapo Januari mwaka 2013.

Wito huo umetolewa wiki hii na Mkurugenzi wa Idara ya Mfuko na Uwezeshaji, BASATA Bw. Angelo Luhala wakati akitoa elimu kwa wadau wa Jukwaa la Sanaa kuhusu ‘Urasimishaji wa Sekta ya Sanaa na Hakimiliki’ kwenye Ukumbi wa Baraza hilo ulioko Ilala Sharif Shamba

Alisema kuwa, wasanii hawana budi kujipanga kuondoka kwenye mazingira ya kufanya kazi kiridhaa na pasipokuwa rasmi bali wanyanyuke na waseme sasa Sanaa ni kazi inayopaswa kupewa heshima yake kama kazi zingine.

“Wasanii tuondoke kwenye ridhaa, tuseme Sanaa ni kazi kama zilivyo kazi zingine, tuunge mkono jitihada za Serikali za urasimishaji sekta ya Sanaa ifikapo mwezi Januari mwakani ili kuipa hadhi sekta hii” alisisitiza Luhala.

Alizitaja faida za urasimishaji sekta ya Sanaa kuwa ni pamoja na kazi zote za Sanaa kutambuliwa kupitia kuwekewa stika maalum na mamlaka ya mapato nchini (TRA) ili kudhibiti uharamia lakini pia kusaidia kupata takwimu sahihi za sekta na kuchangia pato la taifa

“Kuanzia Januari mwakani sekta hii itaanza kurasimishwa. Hii ina maana kuwa, kazi za wasanii zitawekewa stika na TRA ili kudhibiti uharamia. Aidha, mapato yatokanayo na Sekta ya Sanaa yatakuwa bayana kwa Serikali ili kurahisisha upatikanaji wa takwimu na kupanga mipango ya maendeleo ya Wasanii” aliongeza Luhala.

Alizidi kueleza kuwa, zoezi la urasimishaji sekta ya Sanaa ambalo limekuwa likipigiwa chapuo na wasanii wenyewe halitakuwa na maana kama wasanii hawatajitokeza kwa nguvu zote na kuunga mkono juhudi za Serikali.

Mbali na Wasanii, Luhala alizitaja kumbi za Sanaa na burudani, makampuni ya ukuzaji sanaa (mapromota), vikundi vya Sanaa, studio za kurekodia muziki na filamu, wachoraji ramani za majengo na wapigapicha kama wadau wengine wanaotakiwa kurasimishwa kupitia kusajiliwa na kupewa vibali.

Kwa upande wa wadau waliochangia mjadala huo walipongeza hatua hiyo ya Serikali kuona umuhimu wa kurasimisha sekta ya Sanaa lakini wakahoji zoezi hilo kugusa Sanaa za filamu na muziki pekee.

“Tunaipongeza Serikali kwa kujipanga kurasimisha Sekta ya Sanaa lakini ni vema Sanaa za Ufundi na Maonesho nazo zikahusishwa kwenye mchakato huu badala ya filamu na muziki pekee” alishauri NKwama Balanga.