Sunday, August 12, 2012

DK. ULIMBOKA AREJEA, ATOA NENO ZITO

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka, ametua nchini leo mchana kisha kutoa neno zito.
Dk. Ulimboka, aliwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, saa 8:00 mchana, akitokea nchini Afrika Kusini, alipokwenda kwa matibabu.
Madaktari wenzake na wananchi wengine, walimlaki kwa mabango yaliyosomeka:
“Dk. Ulimboka karibu nyumbani.”
“Dk. Ulimboka, damu yako iliyomwagika inaamsha ari ya wananchi kudai haki ya afya.”
“Dk. Ulimboka wewe ni mpigania haki ya afya bora kwa wananchi wote. Mungu na Watanzania wote tuko nawe.”
Kwa upande mwingine, Dk. Ulimboka baada ya kukuta umati mkubwa uwanjani, alishindwa kujizuia, hivyo akatoa machozi kisha akasema: “Nawashukuru sana Watanzania kwa kuwa pamoja na mimi kwa maombi, sasa nimerejea nikiwa na afya njema, mapambano yanaendelea.”
Huku uwanja wa ndege ukiwa umepambwa na mabango mengi ya kumpamba na kumuunga mkono, Dk. Ulimboka aliongeza: “Watu wacheze na watu lakini wasicheze na Mungu, hasa Mungu wangu mimi.”
Juni 26, mwaka huu, Dk. Ulimboka alitekwa na watu wasiojulikana, kupigwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili, kisha kutupwa katika Msitu wa Mabwepande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Ulimboka, alitekwa wakati akiwa anaratibu mgomo wa madaktari na katika utekaji huo, alidaiwa kuvunjwa mbavu, miguu yote miwili, kung’olewa meno yote ya mbele na kuumizwa vibaya katika sehemu mbalimbali za mwili wake.