Sunday, July 8, 2012

Kampeni ya kulipamba taifa na sanaa za nyumbani

WADAU mbalimbali nchini, hususan viongozi wa kitaifa na kidini, wanasiasa na wamiliki wa majengo mbalimbali, wameombwa kuunga mkono kampeni ya kulipamba taifa na kazi za Sanaa za Kitanzania inayotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.
Akizungumza katikati ya wiki hii kwenye mwendelezo wa vikao vya maandalizi ya kampeni hiyo, Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi nchini, Adrian Nyangamalle, alisema kuwa, uungwaji mkono wa wadau hao, utalifanya taifa kupendeza na kuwa kivutio kwa kila mtu.
“Tunategemea kwa kiwango kikubwa uungwaji mkono kutoka kwa wadau hasa viongozi wetu wa kitaifa, lengo ni kumfanya kila mtanzania aone fahari kwa kupamba na Sanaa za nyumbani lakini pia afurahie mandhari nzuri ya taifa lake,” alisema Nyangamalle.
Kwa mujibu wa Nyangamalle, Tanzania imejaaliwa Sanaa nyingi za mikono, kama za vinyago na michoro, ambazo zina mvuto wa aina yake na zinavuta wageni wengi kuja kuzitazama, hivyo kuzipamba kwenye maeneo yetu ya wazi na maofisi, kutabadili kabisa muonekano wa miji na ofisi.
“Tunalenga kampeni hii isambae, ifike mahali iwe lazima kwa ofisi zetu za umma na maeneo ya wazi kupambwa na sanaa za mikono kutoka nyumbani. Ni wazi viongozi wetu wakiunga mkono tutaleta mabadiliko,” alisisitiza Nyangamalle.