Friday, June 29, 2012

Silaha za msaada zinachangia machafuko Sudan Kusini.

Hii ni kwa mujibu wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu, Amnesty International. Ripoti ya shirika hilo imesema raia wameendelea kuawa na kujeruhiwa kiholela kwenye makabiliano kati ya kundi moja la waasi na jeshi la Sudan Kusini.
Amnesty International inasema silaha kutoka Sudan, mabomu ya kutegwa arthini kutoka China na Vifaru vilivyoagizwa Ukraini zimeendelea kutumiwa nchini humo. Hakuna upande ambao umejibu madai ya ripoti hii.
Kutolewa kwa silaha hizo kulifanyika licha ya kuwepo mkataba wa amani wa mwaka 2005 pamoja na marufuku ya silaha iliyowekewa Sudan nzima.Ripoti ya Amnesty International imenukuu machafuko katika Kaunti ya Mayom Jimbo la Unity.Vifaru vya Jeshi la Sudan Kusini vilitolewa kwa lililokua kundi la SPLA kati ya mwaka 2007 na 2009 kutoka Ukraine na kupitishiwa Kenya.Shirika hilo linaendelea kusema ,kampuni za Ujerumani na Uingereza ndizo zilihusika na usafirishwaji wa silaha hizo.
Imesema kulengwa kiholela kwa kambi za jeshi kumesababisha maafa na majeruhi wengi miongoni mwa raia kinyume na sheria ya kimataifa inayosimamia masuala ya kibinadamu.
Shirika hilo sasa linazitaka serikali kutouza silaha kwa nchi ambazo huenda zikazitumia kutekeleza dhuluma za kibinadamu.Mwandishi wa BBC mjini Khartoum amesema huenda ripoti hii ikazua utata japo shirika lingine linalotathmini utumizi wa silaha limetoa taarifa sawa na hio.
Sudan Kusini ilipata uhuru wake mwezi Julai mwaka jana baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miongo miwili.Japo ilisalia na visima vingi vya mafuta Sudan Kusini imeendelea kutumia mabomba ya Sudan kusafirishia mafuta yake kwa soko la kimataifa.
SOURCE BBC