Monday, July 9, 2012

Bei nyumba za NSSF Kijichi Dar yatajwa

Lauden Mwambona
NYUMBA 300 zilizojengwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) eneo la Kijichi Dar es Salaam zitauzwa  kati ya Sh60milioni na Sh120 milioni, ilifahamika mwishoni mwa wiki.Maofisa wa NSSF walisema hayo walipotoa taarifa za kazi mbalimbali za mfuko kwa watu waliotembelea banda lao kwenye Maonyesho ya Biashara yaliyofikia kilele juzi kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere jijini hapa.

Ofisa Uwekezaji Mkuu wa NSSF, Gerald Sondo alisema ujenzi wa nyumba hizo zinazotofautiana kwa idadi ya vyumba  umekamilika na kwamba hivi sasa wanaendelea na kazi za kuweka umeme, kupeleka maji na kutengeneza barabara.

Sondo alisema uuzwaji wa nyumba hizo utafanywa na Benki ya Commercial Bank Of Africa (CBA) na kwamba benki hiyo imeelekezwa kuwafikiria zaidi wanachama wa NSSF.

“NSSF imeingia makubaliano na CBA itakayowauzia kwa fedha taslimu au kuwakopesha Watanzania hususan wanachama wa NSSF nyumba zilizoko Kijichi wilayani Temeke . Utaratibu wa malipo ni papo kwa papo au kukopesha kwa kipindi kisichozidi  miaka 15’’ alisema.
Naye Ofisa Mwekezaji wa mfuko huo, Sakina Mbiru alifafanua kwamba  kinachotakiwa sasa kwa watu wanaotaka nyumba ni kufungua akaunti kwenye benki hiyo ili kujiweka kwenye  mazingira mazuri ya kufikiriwa kwanza.
Alipoulizwa juu ya kuwapo kwa riba kubwa kupitia benki hiyo, alisema NSSF na benki hiyo wamekubaliana kutoa riba ndogo zaidi kwa mikopo ya nyumba hizo na kwamba bei  ya nyumba hizo imezingatia ubora na thamani ya ardhi Dar es Salaam.

Wakati huohuo, NSSF  hatimaye itaanza kufunga mitambo ya ATM jijini  Dar es Salaam na mikoani mwishoni mwa mwezi huu ili  kuwarahisishia wanachama wake kujua michango  na mambo mengine  muhimu.
Ofisa Mwendeshaji wa mitambo ya kompyuta wa NSSF, Kassim Mwandoro alisema  kwa sasa wamepata ATM 10 na kwamba lengo ni kuzifunga kwenye maeneo yenye wanachama wengi na  maeneo ya mbali hususan migodini ambako kuna wanachama wengi pia.
NSSF ilizindua mpango wake wa Smart Card miaka 10 iliyoita, lakini utekelezaji wake ulikuwa ukisuasua kutokana na sababu ambazo hazikuwa wazi kwa wanachama wengi